Kamishna
wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (katikati)
akizungumza na Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi
wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga,
Arusha, Kilimanjaro na Manyara. Kulia kwake ni Opio Mamu Msimamizi wa
mafunzo katika kanda hiyo na kushoto kwake ni Juma Shaban Meneja
Takwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkoa wa Manyara.
Wadadisi
wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda
ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na
Manyara wakimsikiliza kwa makini Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi.
Hajjat Amina Mrisho Said (hayupo pichani) katika mafunzo ya utafiti huo
yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga.
Kamishna
wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo
wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha
mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara. Mafunzo ya utafiti huo
yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga. (Picha zote na Veronica
Kazimoto - Tanga)
Na.Veronica Kazimoto na Aron Msigwa – Tanga.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imewataka wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa
Serikali, siasa na waandishi wa habari kutumia takwimu sahihi
zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pindi wanapotekeleza majukumu
yao.
Akizungumza
na waaandishi wa habari pamoja na wadadisi wa Madodoso ya utafiti wa
Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi mwaka 2014 kutoka kanda ya kaskazini
leo jijini Tanga Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi kutoka Ofisi ya
Taifa ya Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said amesema kuwa ni jukumu la
kila mtendaji katika eneo lake kuhakikisha kuwa anatumia takwimu sahihi
zinazotolewa na Ofisi hiyo.
Amesema
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye mamlaka na dhamana ya utoaji wa
takwimu za masuala mbalimbali nchini na kuongeza kuwa matumizi ya
takwimu zisizo sahihi yana athari kwa jamii hasa wakati wa kupanga
mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya vijiji mpaka taifa.
Amesema
kuwa takwimu sahihi huwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na
kuongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo ufumbuzi wake unaweza
kupatikana kwa kufanya rejea ya takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu.
“Takwimu
ni muhimu sana katika kupanga namna ya kukabiliana na matatizo na
majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii kama mafuriko, njaa, masuala
ya ardhi na elimu ambayo kimsingi yanahitaji matumizi ya takwimu sahihi
ili kujua kiwango halisi cha ukubwa wa tatizo na namna ya kupata
suluhisho la kudumu kwa wananchi husika.
Amesema
ni vema wadau wanaotumia takwimu kwenye majukwaa mbalimbali na
waandishi wa habari kujenga tabia ya kuwasiliana na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu kabla ya kutoa takwimu walizonazo ili kupata ukweli wa hali
halisi.
“Natoa
wito kwa wadau mbalimbali na waandishi wa habari kuhakikisha kuwa
mnapata takwimu sahihi hata kama mmezipata kutoka kwa viongozi,
tafadhali hakikisheni mnapitia mamlaka husika kupata ukweli wa takwimu
hizo ili kuepuka kutoa takwimu zisizo sahihi”, Amesisitiza Kamishna wa
Sensa.
Ametoa
wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti ya Ofisi ya Taifa ya
Takwimu ikiwa ni moja ya chanzo sahihi cha habari katika masuala yote
yahusuyo takwimu na rejea sahihi na kuongeza kuwa takwimu zote
zinazotumika kutengeneza sera za taifa za mipango ya maendeleo zinatoka
katika chanzo kimoja tu ambacho ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Katika
hatua nyingine Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said ametoa wito kwa Maofisa wa Takwimu
walio katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kutumia vikao mbalimbali
vinavyofanyika katika Halmashauri na mikoa kutoa elimu ya matumizi ya
takwimu zilizopo ili waweze kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo na
kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Amesema
takwimu zilizopo lazima zitafsiriwe na jukumu hilo lazima lifanywe na
wawakilishi hao wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu walio katika mikoa
mbalimbali nchini na kuongeza kuwa wataalam hao kwa kushirikiana na
viongozi wengine wa halmashauri wana jukumu la kutoa elimu kwa makundi
mbalimbali ya jamii hasa vijana ili waweze kujiajiri na kutumia fursa
zilizopo katika maeneo yao ili kupunguza utegemezi.
“Naomba
mtumie vikao hivyo vya hamashauri kutoa elimu kwa sababu tayari ninyi
mnazo takwimu, vikao vya halmashauri huwa vinahusisha viongozi
mbalimbali wa Serikali na jamii hivyo mnaweza kabisa kushauri na
kushawishi kwa viongozi hao kutumia takwimu sahihi ili kuondoa matatizo
mbalimbali likiwemo tatizo la ajira kwa vijana na kuondoa utegemezi kwa
kuwajengengea uwezo vijana wasio na ajira kujiajiri wenyewe”, amesema
Kamishna.
Aidha
ametoa wito kwa watafiti na wadadisi wa Madodoso ya Watu Wenye Uwezo wa
Kufanya Kazi 2014 watakaoendesha zoezi la utafiti wa idadi ya watu wenye
uwezo wa kufanya kazi kutoa elimu kwa vijana ambao hawana kazi katika
maeneo yote watakayopita ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi pia
kuwashauri kujiunga na vyuo vya ufundi Stadi (VETA) vilivyopo katika
maeneo mbalimbali nchini ili waweze kujiajiri na kuondoa wimbi la
utegemezi.
Post a Comment