Mgeni
rasmi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kigamboni Ndugu Faustine
Ndungulile akifungua rasmi Baraza la kazi la UVCCM (W) Temeke mbele ya
Wajumbe (hawapo pichani) lililofanyika kwenye ukumbi wa Malaika uliopo
Kata ya vijibweni, Jimbo la Kigamboni.
**********
Na
Emmanuel J. Shilatu
Mbunge
wa Kigamboni Mhe. Faustine Ndungulile ameanika siri na aina mpya ya wauzaji wa
madawa ya kulevya wanayoitumia katika kupanua wigo wa watumiaji wa madawa ya
kulevya Duniani kupitia watoto wadogo.
Mhe.
Ndungulile aliyasema hayo wakati akifungua Baraza la Vijana la Umoja wa vijana
wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia wilaya ya Temeke uliofanyika katika
ukumbi wa Malaika ambapo alibainisha bayana kuwa wauzaji wa madawa ya kulevya
wamekuja na mtindo mpya wa kuwafundisha watoto wadogo kutumia madawa ya kulevya
kupitia kwenye vyakula wanavyopewa wakiwa mashuleni pamoja na kwenye pipi
ambazo watoto hao wanapozilamba taratibu huanza kujifunza kutumia madawa ya
kulevya na hata katika siku za usoni inawawia vigumu watoto hao kuacha matumizi
ya madawa hayo.
“Wauzaji
wa madawa ya kulevya ni watu hatari sana kwani siku hizi wameanzisha mtindo wa
kuwachanganyia watoto wadogo kwenye vyakula pamoja na kuyapaka madawa hayo ya
kulevya kwenye pipi ambazo watoto hao wanapozilamba huanza kujifunza matumizi
ya madawa ya kulevya tangu wakiwa watoto na ni ngumu kuchomoka katika mtego wa
matumizi ya madawa hayo katika maisha yao”, alisema Mhe. Ndugulile.
Kama
haitoshi Mhe. Ndungulile alianika bayana matatizo makubwa yanayowasibu vijana
kwa sasa kuwa ni madawa ya kulevya pamoja na maambukizi ya virusi vya ukimwi
ambapo alibainisha waziwazi kuwa nguvu kazi ya taifa la leo imekuwa rehani
kupitia mitego hiyo.
Mbunge
huyo wa Kigamboni ambaye kitaaluma ni Daktari aliweka waziwazi kuwa licha ya
takwimu za kushuka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi kushuka kutoka asilimia
7 mpaka asilimia 5.1 bado tatizo ni kubwa kupita maelezo kwa vijana nchini.
“Kati
ya vijana wa kike watatu wanaotumia madawa ya kulevya, wawili kati yao ambao ni
asilimia 67 wameathirika na virusi vya ukimwi. Halikadhalika kwa upande wa
vijana wa kiume wawili wanaotumia madawa ya kulevya, mmojawao ambaye ni
asilimia 50 ana maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hali ni mbaya sana kwa vijana.”
Alisema Mhe. Ndungulile.
Mbunge
huyo wa Kigamboni aliwaasa wajumbe hao wa Baraza la UVCCM (W) Temeke na vijana
wote nchini kuwa mbali na matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake
wajibiidishe zaidi katika kufanya mambo yenye faida kwao kupitia shughuli za
kiuchumi kwa kuchangamkia fursa zilizopo.
Post a Comment