Twiga. |
Kesi utoroshwaji wa twiga kwenda Uarabuni,
imekwama baada ya mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Kamran Ahmed,
kuugua ghafla muda mfupi kabla ya kufika mahakamani hapo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi, jana ililazimika kuahirisha
kesi hiyo baada Wakili wa mshitakiwa huyo, Edmund Ngemela, kuieleza
mahakama hiyo kwamba sukari ya mshitakiwa huyo ilipanda na kusababisha
ashindwe kufika mahakamani kuendelea na kesi inayomkabili.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Simoni Kobelo na mawakili wa pande
zote mbili, Ngemela alidai hali ya afya ya mteja wake, ilisababisha
ashindwe kufika mahakamani hapo.
"Mheshimiwa Hakimu kesi hii ilikuja kwa ajili ya kuendelea na
mashahidi upande wa mashitaka, lakini niiombe mahakama yako tukufu,
iahirishe kwani mteja wangu, sukari imepanda kuliko kiwango cha
kawaida," alisema.
Katika kesi hiyo iliyozungumzwa katika mahakama ya ndani, tofauti na
juzi ambapo ilisikilizwa katika mahakama ya wazi, mawakili wa Serikali
hawakuwa na pingamizi dhidi ya maombi hayo na kutaka mahakama kufuata
taratibu zake.
Kesi hiyo ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi
ambapo upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili Evetha Mushi, Joseph
Maugo na Steven Mwanasenjele, ulifika kwa ajili ya kuongoza mashahidi
Tayari upande wa mashitaka umeleta mashahidi 21 na
jana ilikua ni mwendelezo wa mashahidi wake kufika mahakamani hapo.
Kutokana na maombi hayo, Hakimu Kobelo aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 21, 24 na 25 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari nje ya mahakama, Wakili Ngemela alisema
mteja wake alimuacha nyumbani kwake asubuhi, akijiandaa kwenda hospitali
kutazama zaidi afya yake.
Hata hivyo kesi hiyo ambayo ilipangwa kusikilizwa kuanzia saa 3.00
asubuhi katika mahakama ya wazi, wanahabari walijikuta wakisubiri hadi
saa 4.55 asubuhi bila kufahamu kilichoendelea hadi walipotaarifiwa kesi
inakaribia kuahirishwa katika mahakama ya ndani.
Juzi shahidi wa 20, Robert Nyanda alielezea alivyopokea maelekezo
kutoka kwa bosi wake Rosemary Israel ya kuandaa vifaa vya kuinua vitu
vizito kwa ajili ya kupakia wanyama hao katika ndege ya Qatar.
Aidha, shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa siku ya tukio
wanyama hao walipakiwa katika ndege hiyo saa nane usiku na waliletwa
uwanjani hapo na lori aina ya Fuso pamoja na vijana maalumu kwa ajili ya
kusaidia upakiaji wake katika ndege
Post a Comment