Ni kujadili namna ya kupunguza vifo vya wajawazito
Na Mwandishi Wetu
MUUNGANO
wa Utepe Mweupe (White Ribbon Allience for Safe Motherhood Tanzania)
wiki hii walikutana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda na
kujadiliana namna ya Serikali inavyoweza kuokoa maisha ya wajawazito
hasa wakati wa kujifungua. Pia mkutano huo ulirejea ahadi ambazo
zilishatolewa na serikali kwamba kufikia mwaka 2015 asilimia 50 ya vituo
vyote vya afya nchini Tanzania vitakuwa vinatoa huduma za dharura
zikiwemo upasuaji na damu salama kwa ajili ya kusaidia wajawazito
nyakati za kujifungua.
Kupitia
kampeni ya ‘Wajibika Mama Aishi’ iliyochini ya Muungano wa Utepe Mweupe
inayolenga kuikumbusha Serikali ahadi yake ya kuhakikisha asilimia 50
ya vituo vya afya vinatoa huduma za dharura; walimuomba Waziri Pinda
atoe agizo kwa Serikali kuweka kipengere cha huduma za dharura katika
vituo vya afya na kutengewa bajeti mahususi kwenye bajeti ya Serikali ya
mwaka 2014/15.
Takwimu
zinaonesha kwa Tanzania kila siku wanawake 24 hupoteza maisha kutokana
na matatizo ya uzazi. Lakini wanawake wengi wanaopata matatizo
yanayosababisha kupoteza maisha, wangeweza kuokolewa pale tu wanapopata
huduma za uzazi za dharura. Njia pekee ya kuepusha vifo visivyo vya
lazima vitokanavyo na matatizo ya uzazi ni wanawake kupata kwa wakati
huduma za dharura kama vile upasuaji na damu salama katika vituo vya
afya wanakojifungulia pale inapobidi.
Katika
Mkutano huo, Mkurugenzi wa Shirika la Evidence For Action Tanzania,
Craig Ferrah alisema vifo 24 vya akina mama vinavyotokea kila siku
nchini haina tofauti na ajali za kila siku za ndege na kuongeza kuwa ipo
haja ya Serikali kuweka kuweka mkakati wa kukomesha ajali hizo ndani ya
saa 48. Hata hivyo ombi kuu kutoka muungano huo kwa Waziri Mkuu
lilikuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa iagize kuwepo wa kipengele mahususi cha bajeti ya
huduma za uzazi za dharura zikiwemo upasuaji na damu salama katika vituo
vya afya kwenye bajeti ya mwaka 2014/2015.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu Pinda aliguswa na ukubwa wa tatizo hilo la vifo
vya wajawazito nchini na kuelezea umuhimu wa kutafutia namna ya
kukabiliana na tatizo ambalo linaelekea kuwa la kudumu. Waziri Pinda
aliridhia moja kwa moja ombi kutokana na kuguswa na takwimu zilizotolewa
juu ya vifo vya wajawazito na kukubali kuwa Serikali itatenga bajeti
mahususi ambayo itaelekezwa kuhimarisha vituo vya afya nchini ili viweze
kutoa huduma ya dharura yaani damu salama, upasuaji pamoja na wataalamu
na vifaa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Mkutano
huo pia ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka mashirika ya; Jhpiego, CARE,
Plan International (Wazazi na Mwana), Evidence4Action, Medical Women
Association of Tanzania na Chama cha Wakunga Tanzania walihudhuria kama
sehemu ya Muungano wa Utepe Mweupe (White Ribbon Allience for Safe
Motherhood Tanzania).


Post a Comment