Ingawa tendo la ndoa lisipofanywa kwa kuzingatia kanuni na
taratibu, sambamba na umakini, linaweza kusababisha maradhi, lakini kwa
wanandoa, tendo hilo linatajwa kuwa na manufaa mengi kiafya tofauti na
faraja ya kawaida iliyozoeleka kwa wengi.
Imefahamika kuwa tendo hili likifanyika ipasavyo
husaidia kuondoa msongo wa mawazo, maradhi ya moyo, maumivu ya kichwa
yasiyokoma na kupunguza kasi ya saratani ya tezi dume.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya
Tiba Muhimbili (Muhas), Dk Yahya Kishashu anasema inategemea tendo
linafanywa na nani na mhusika yupo kwenye mazingira gani.
“Kwa mfano, tendo la ndoa linaondoa msongo wa
mawazo iwapo unayetenda naye unampenda na amekupa maandalizi mazuri.
Sidhani kama alimradi utende hilo tendo na yeyote litakusaidia,” anasema
mtaalamu huyo.
Anaongeza kuwa ndiyo maana baadhi ya watu
wanatoka nje ya ndoa zao kwa sababu si mara zote tendo la ndoa
linawafurahisha wanandoa.
“Wakati mwingine tendo hilo laweza kuwa karaha kwao,” anasema
Mazoezi
Si hivyo tu, utafiti uliofanyika Canada hivi
karibuni umebainisha kuwa kufanya tendo la ndoa kwa kipindi cha dakika
25 kwa wanamume kunachoma kalori 100 na kwa wanawake kalori 69.
Tendo hilo likifanyika kwa nusu saa, linaweza
kupunguza kalori za mwili kuliko kutembea kwenye mashine ya mazoezi ya
‘treadmill’.
“Ni sawa na kucheza mpira wa tenisi au kutembea
ukipanda mlima kwa dakika 20 au kucheza gofu kwa kasi kwa dakika 33 au
zoezi la yoga kwa dakika 40,” sehemu ya utafiti hiyo inasema.
Utafiti huo wa Canada ulishabihiana na kampeni
iliyofanywa na Taasisi ya Moyo ya Uingereza ambayo ilisema kuwa dakika
30 za tendo la ndoa kwa siku ni muhimu kama mazoezi ya kutembea kwa
mashine.
Kwa undani zaidi utafiti huo ulichambua na kusema kuwa, tendo la ndoa, lina manufaa kwa moyo na mapafu.
Inaelezwa kuwa vichocheo vinavyotoka baada ya tendo la ndoa
vinasaidia kupunguza kiwango cha msongo wa mawazo na kuongeza
uzalishaji wa seli mpya za ubongo.
Kuhusu mazoezi, Dk Kishashu anasema anakubaliana
na utafiti huo na kusema kuwa ni kweli tendo hilo linasaidia kupunguza
kalori, lakini linapofanyika mara nyingi zaidi linazeesha.
Hata hivyo, wanasayansi wanalipa uzito mdogo tendo
hilo katika muktadha wa ujenzi wa hisia na mwili na kuwa halisisitizwi
vya kutosha kama aina mojawapo ya mazoezi.
Tiba kwa moyo, mapafu na ubongo
Inaelezwa kuwa tendo la ndoa, linasaidia kuondoa msongo wa mawazo hivyo kupunguza hatari ya maradhi ya moyo.
Si hivyo tu, bali tendo hilo husaidia mapafu kufanya kazi yake vyema, kuingiza na kutoa hewa chafu.
Kitaalamu, upo mchakato uitwao ‘Neurogenesis’
ambao husaidia kulinda seli za ubongo zinazokufa kutokana na uzee. Kuna
eneo kwenye ubongo linaloitwa ‘hippocampus’ ambalo ni eneo
linalotengeneza kumbukumbu.
“Kazi kubwa inafanyika kwenye ubongo, wakati wa
tendo la ndoa, kiasi kikubwa cha viamsha raha huanzia kwenye ubongo na
kuleta taarifa kwenye maeneo mengine ya mwili.
Ndiyo maana watu wengi hupotea kiufahamu wakati wa kilele” anasema Dk Gosh, ambaye ni mtafiti.
Hata hivyo, wanaume ambao wanaendelea na tendo la
ndoa mara kwa mara hadi wanapofikisha miaka 50 na zaidi, kwa maana ya
kutoa mbegu za kiume mara kumi kwa mwezi, wapo katika hatari ndogo ya
kupata saratani ya tezi dume. Inaelezwa kuwa mbegu za kiume hazitakiwi
kukaa mwilini kwa muda mrefu.Zinatakiwa zitolewe mara kwa mara ili
kuzifanya seli mpya zizalishwe. Ni kama kusafisha mpira, inasaidia
kusitisha ujenzi wa seli za zamani ambazo zaweza kuwa chanzo cha
saratani.
Kwa wanawake, tendo la ndoa husaidia kuundwa kwa
misuli ya nyonga ambapo misuli hiyo ikiwa imara huondoa hatari ya
kushindwa kuzuia mkojo,(urine incotinence) jambo linaloathiri mwanamke
mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka zaidi ya 50.
“ Wakati wa tendo la ndoa, kwa kawaida sakafu ya
nyonga za mwanamke hubana na kuachia. Hii husababisha misuli hiyo kuwa
imara’ anasema mtafiti huyo.
Hata hivyo, utafiti wa Chuo Kikuu cha Nottingham nchini
Uingereza unaeleza kuwa, wanaume wanaofanya tendo hilo na kumwaga
mbegu mara 20 hadi 30 kwa mwezi, wapo katika hatari ya kupata saratani
ya tezi dume kwa sababu ya umri wao .
Kuondoa maumivu ya kichwa
Utafiti mwingine umebaini kuwa, wanawake wenye
umri mdogo hukumbwa na msongo wa mawazo iwapo hawatafanya tendo la ndoa
kwa muda mrefu.
Wanawake hao, wanapofika kilele cha tendo hilo, damu hutembea kutoka kwenye ubongo, jambo ambalo huondoa maumivu ya kichwa.
Dk Innocent Mosha, Mchunguzi wa magonjwa wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili anasema kuwa inawezekana kuwa tendo la
ndoa likasaidia kuondoa msongo wa mawazo iwapo mtu hajalifanya kwa muda
mrefu na yupo katika hali kubwa ya uhitaji.
“Kama mtu hajafanya tendo hilo muda mrefu na hivyo amelikamia, basi akilifanya litamwondolea msongo wa mawazo,” anasema
Anasema mtu ambaye anahitaji kufanya tendo hilo
na hajalipata, aghalabu huwa na msongo wa mawazo lakini kama huliwazi
hawezi kuwa na msongo.
Kwenye utafiti huo, wanawake 83 wenye maradhi ya kichwa walipata nafuu kubwa baada ya kumaliza tendo la ndoa.
Ukaribu/ upendo
Mwanasaikolojia, wa Chuo Kikuu cha Dodoma,
Modesta Kimonga anasema ni kweli kuwa tendo la ndoa linaleta faraja
inayoondoa msongo wa mawazo.
Anasema hali hiyo inatokana na nadharia au mfumo wa uambatano katika saikolojia au ‘attachement theory’
“Hii ‘attachment theory’ ipo kwa watoto
wanaponyonya maziwa ya mama zao, na kwa watu wazima ni kwenye tendo la
ndoa ambalo linaleta faraja na ukaribu,” anasema.
Anaongeza: “Faraja hupatikana baada ya wanandoa kutenda tendo hilo na huweza kuondoa kabisa mawazo kichwani au huzuni.”
Watafiti walibaini kuwa vichocheo vya ‘oxtocin’
vinavyotolewa wakati wa tendo hilo husaidia hisia za upendo na
mshikamano kwenye uhusiano ya muda mrefu.
Lipo ongezeko kubwa la kemikali ya ‘oxtocin’ kwa
wanawake na wanaume baada ya kumaliza tendo la ndoa ambalo husaidia
kukuza uhusiano na ukaribu wao.
Wanaume kulala baada ya tendo la ndoa
Utafiti wa jarida la Sayansi ya Mishipa ya Fahamu
na Tabia uliochapishwa mwaka 2012 umebaini kuwa, dawa za usingizi
hufanya kazi sawa na tendo la ndoa kwa wanaume.
Eneo la mbele la ubongo ‘pre –frontal cortex’,
ambalo linahusiana na ufahamu, au umakini wa kiakili, huzima au
kufungwa baada ya kumaliza tendo hilo.
Kwa baadhi ya utafiti, wanaume kumaliza tendo la
ndoa, ni sawa na kunywa dawa za usingizi za ‘diazepam’ zenye ukubwa wa
miligramu mbili.
Pia, vichocheo vinavyotoka baada ya tendo hilo
kama ‘melatonin,’ ‘oxytocin’ na ‘vasopresin’, zinamsababisha mwanaume
apate usingizi mzito.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment