**********
Waraka huo wa kurasa 22 unaoainisha mambo yenye masilahi kwa chama hicho, unawataka wajumbe wake kuutetea bungeni.
Gazeti hili limefanikiwa kuona waraka huo, ambao
pamoja na mambo mengine, umetoa mapendekezo katika ibara 42 za Rasimu ya
Katiba ya Tume na kupangua hoja nyingi.
Katika miongoni mwa hoja hizo, chama hicho
kimesisitiza muundo wa Muungano wa Serikali mbili lakini kikapendekeza
kuwapo Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu waraka huo, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliukana akisema pamoja na
msimamo wa chama hicho kuwa ni Serikali mbili, hakijafikia hatua ya kuwa
na waraka.
Alisema vikao vya juu vya chama huwa havitoi
waraka, bali msimamo na kwamba vyombo vingine vya chama ndivyo hutoa
waraka, lakini hadi sasa havijafikia hatua hiyo.
Alisema kuwa alipoeleza maazimio ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alitaja msimamo wa chama hicho kuwa ni
Serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hakutaja maboresho hayo hata pale
alipoulizwa na waandishi wa habari kwa sababu hayakuwa yamekamilika.
Hata hivyo, wajumbe watatu wa NEC kwa nyakati
tofauti waliomba wasitajwe gazetini walisema mambo yaliyomo kwenye
waraka huo ndiyo waliyokubaliana lakini hakuwa na uhakika kama
ulishasambazwa.
Kwa mujibu wa waraka huo, chama hicho kinadaiwa
kuainisha mambo kiliyopendekeza katika Rasimu ya Kwanza na jinsi
yalivyoshughulikiwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Pia, kimeeleza mambo mengine mapya na kubainisha kasoro zake, ikiwamo utata katika mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
Waraka huo pia unazungumzia sura mpya ya 17 katika
Rasimu ya Katiba, ukisema inazungumzia mambo ya mpito kuelekea kupata
Katiba Mpya, lakini gharama za utekelezaji wake hazitabiriki.
Sababu za Serikali mbili
Katika waraka huo, CCM kinadaiwa kueleza kuwa
mapendekezo yake kuhusu muundo wa serikali mbili hayatokani na sera yake
pekee, bali pia udhaifu uliojionyesha katika pendekezo la muundo wa
Serikali tatu.
“Hivyo basi, CCM inapendekeza kwamba mfumo wa serikali mbili
ufanyiwe marekebisho ambayo yatashughulikia changamoto zilizopo,”
imesema sehemu ya waraka huo.
Wakati CCM kikitaka Muungano wa serikali mbili,
Rasimu ya Pili ya Tume inapendekeza serikali tatu, sawa na zile
zinazopigiwa chapuo na vyama vya Chadema na CUF.
Idadi ya Serikali katika muundo mpya wa Muungano,
bado ni changamoto kutokana na hatua ya wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kugawanyika katika makundi yenye mitazamo tofauti.
Makamu wa Rais
Katika mfumo huo wa serikali mbili, waraka huo
umependekeza Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais bila kujali kama Rais
wa Jamhuri ya Muungano anatoka Bara au visiwani humo.
“Rais wa Zanzibar katika Muungano, awe Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa na msaidizi wake kwa masuala
ya Zanzibar na mmoja wa viongozi wakuu wa nchi,” imesema sehemu ya
waraka huo na kuongeza:
“Hii itaongeza na kuweka wazi madaraka ya Rais wa
Zanzibar ndani ya Serikali ya Muungano na nje ya nchi,” imesema sehemu
ya waraka huo.
Muundo wa Bunge
Kuhusu Bunge, waraka huo unapendekeza kuwe na
Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara kwa ajili ya kushughulikia
masuala ya Bara tu.
“Katika pendekezo hili, majimbo ya Jamhuri ya
Muungano yaundwe upya na majimbo ya uchaguzi ya Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar yawe ndiyo hayohayo majimbo ya uchaguzi ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano,” ulisema waraka huo.
Waraka huo umependekeza Bunge la Muungano wakati
linajadili mambo ya Muungano, wabunge wote washiriki majadiliano na
inapofika kujadili mambo ya Tanzania Bara, washiriki wabunge wanaotoka
Bara tu.
“Kama Spika anatoka sehemu moja ya Muungano, Naibu
wake atatoka upande wa pili na wakati wa vikao vya masuala ya Bara
Spika/Naibu Spika anayetoka Bara ndiye atakayeendesha kikao,” sehemu ya
waraka huo inasema.
Waraka huo umependekeza masuala yasiyokuwa ya Muungano, kushughulikiwa na wabunge wa Tanzania Bara pekee.
Muundo wa mawaziri
Waraka huo umependekeza wajumbe wa Bunge la
Muungano kuwa mawaziri wa wizara za mambo ya Muungano tu na wizara
zisizo za Muungano ziongozwe na wabunge wanaotoka Tanzania Bara tu.
Pia umependekeza orodha ya mambo ya Muungano
ambayo yatakuwa katika Katiba na mambo yasiyokuwa ya Muungano
yaorodheshwe katika sheria itakayoainisha pia usimamizi, utekelezaji na
gharama zake.
Mahakama
Kwa upande wa muundo wa Mahakama ya Juu, waraka umependekeza ndani ya mahakama hiyo kuwe na kitengo cha masuala ya Katiba tu.
Kuhusu misaada na mikopo nafuu kutoka kwa
wahisani, umependekeza Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya
Zanzibar, zijadili kwa kina kanuni ya mgawanyo wa fedha zinazotokana na
vyanzo hivyo.
“Kuwekwe utaratibu wa kisheria wa kutenganisha
misaada inayoelekezwa kwenye miradi ya Muungano na isiyokuwa ya
Muungano,” ilisema sehemu ya waraka huo.
Usimamizi wa Muungano
Waraka huo umependekeza kuwapo kwa Tume ya
Usimamizi na Uratibu wa mambo ya Muungano kikatiba na uendeshaji wake,
kadhalika na mwenendo wa sasa wa vikao vya pamoja vinavyohusu kero za
Muungano.
“Uratibu na usimamizi wa masuala ya Muungano
uwekwe kisheria na Tume ipewe mamlaka ya kuzisimamia taasisi zote za
Muungano katika makubaliano yatakayofikiwa na pande zote mbili,” unasema
waraka huo.
Kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha, waraka huo unasema
tume hiyo ambayo imetamkwa katika Katiba na kupitishwa na Sheria ya
Bunge, imeshaundwa na mamlaka yake yanafahamika.
“Tunapendekeza Tume hii ipewe nguvu zaidi, iwekewe mfumo
madhubuti wa kuiendesha na kuisimamia kwa karibu. Mapendekezo
yanayotolewa na Tume yashughulikiwe na serikali zote mbili kwa haraka
ili kama hakuna kikwazo, mapendekezo yake yatekelezwe bila kuchukua muda
mrefu,” unasema.
Pia waraka huo umependekeza kufunguliwa kwa
akaunti ya pamoja ya fedha zitokanazo na mapato ya vyanzo vya Muungano,
kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kuwapo kwa utaratibu wa kisheria utakaoelekeza uendeshaji wa akaunti
hiyo na kuweka mgawanyo wa mapato hayo kwa pande mbili za Muungano.
“Hii itasaidia sana kuwianisha uchumi wa pande
hizo mbili. Sheria kuhusu utaratibu huo isimamiwe na Tume ya U husiano
na Uratibu kama ilivyopendekezwa katika rasimu,” waraka huo unasema.
MWANANCHI
Post a Comment