Afrika Kusini imetoa onyo kali kwa Rwanda huku mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo ukiendelea kutokota.
Hii ni baada ya hali ya kulipiza kisasi kati ya nchi hizo katika kuwafurusha mabalozi wao.
Waziri
wa sheria wa Afrika Kusini, Jeff Radebe, amesema kuwa nchi hio
haitastahamili vitendo vinavyokiuka sheria katika ardhi yake kama
mashambulizi dhidi ya maadui wa Rwanda wanaoishi nchini humo.
Alikuwa
akigusia madai ya njama ya kumuua Generali Kayumba Nyamwasa, aliyekuwa
anahudumu katika jeshi la Rwanda zamani ingawa sasa anaishi nchini
Afrika Kusini.
Rwanda
iliwafurusha wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini baada ya serikali ya
Afrika Kusini kuwafukuza wafanyakazi watatu wa ubalozi wa Rwanda na
mmoja wa Burundi nchini humo baada ya kuwahusisha na njama ya kutaka
kumuua Nyamwasa.
Wakati
huohuo, Mjumbe maalum wa Rais Barack Obama katika kanda ya maziwa
makuu, Russ Feingold amesema kuwa nchi za Rwanda na Afrika Kusini hazina
budi kumaliza mzozo kati yao kwa njia za kidiplomasia.
Mjumbe huyo aliyasema hayo mjini Kigali baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Feingold
amesema Marekani inafuatilia kwa karibu karibu kundi la FDLR akilitaja
kama moja ya makundi hatari katika eneo hilo la maziwa makuu.Chanzo BBC
Swahili
Post a Comment