Mhe. Sitta
akionesha fomu aliyochukua jana. Kushoto ni Mhe. Dk Kigwangala na kulia
ni Mjumbe wa Bunge hilo Bw. Paul Makonda. (picha zote: Hassan
Silayo/MAELEZO).Samuel Sitta
ambaye ni miongoni mwa wajumbe watatu wa Bunge Maalumu la Katiba ambao
walichukua fomu jana, ameahidi kusimamia utaratibu ambao hauna upendeleo
utakaowezesha Watanzania kupata Katiba bora.
Waliochukua fomu hizo jana ni Dk Terezya Huvisa, John Lifa Chipaka na
Hashimu Rungwe ambao wanatarajia kurejesha fomu hizo leo saa nne asubuhi
na uchaguzi wa Mwenyekiti utafanyika leo jioni.
Sitta alisema anaamini kuwa ndani ya Bunge, kuna watu wenye itikadi
mbalimbali hasa kuhusu mtazamo wa Muungano unaostahili, lakini licha ya
chama chake kuweka msimamo wa kutaka serikali mbili, yeye atakuwa
mwamuzi atakayesimamia hoja zote na hoja bora ndiyo itakayopita.
Sitta, ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki, alisema itakuwa heshima
kwake iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo na akaahidi kulinda heshima
kwa kuepuka kuwa Mwenyekiti wa ovyo.
"Najua dunia nzima inaangalia mchakato huu, mimi naogopa kuwa Mwenyekiti
wa ovyo, ndio maana nasema nitatumia akili zangu na uzoefu wangu na
nitamwomba Mungu aniwezeshe niwe msimamizi bora," alisema Sitta baada ya
kuchukua fomu.
Suala kubwa ambalo ameahidi kutoa, ni Katiba nzuri itakayoondoa kero za
Muungano, lakini Katiba ambayo itawezesha kufutwa kwa sheria mbovu
ambazo zinatoa mianya ya waovu kuachiwa huru na Mahakama.
Sitta alichukua fomu hizo jana mchana katika ofisi za Bunge na
kukabidhiwa na Ofisa wa Bunge, Lydia Mwapyina huku akiwa ameambatana na
wapambe wake ambao ni Paul Makonda na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis
Kigwangalah.
Sitta, ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge na kauli mbiu yake ya spidi na
viwango, aliahidi kuendeleza mfumo huo kwa kuhakikisha wabunge wote
ambao wako ndani ya Bunge hilo, wanapata nafasi ya kuchangia wakiwemo
wateule 201 wa Rais.
Sitta alisema amechukua fomu hiyo kwa vile anaamini kuwa uzoefu wake
akiwa Spika wa Bunge la tisa na kwa kuwa umri wake ambao umeongezeka, ni
wazi kuwa busara itakuwa imeongezeka mara dufu.
Aliahidi kufanya vizuri zaidi ya alipokuwa Spika na kwamba atatumia
nafasi hiyo na kuendesha mijadala kwa haki na usawa, bila kutawaliwa na
hisia za vyama vya siasa wala matakwa ya watu binafsi kwa maslahi yao.
"Ninajua wazi wapo wajumbe humu ndani ya Bunge ambao sio wazoefu wa
mambo ya kibunge; lakini kutokana na jinsi walivyoona mijadala
ilivyokuwa ikifanyika wakati wa kujadili kanuni, wamepata uzoefu.
"Nitajaribu kuwapa kipaumbele waliokosa nafasi ya kuzungumza mara kwa
mara katika vikao, ili kutoa nafasi kwa mawazo yao na michango yao
isikike," alisema Sitta.
Alisema uendeshaji wa Bunge hilo utakuwa ni rahisi kutokana na kuwepo
kwa kamati mbalimbali za Bunge zenye wajumbe 53, zitakazokutana na
atazisimamia ili kuhakikisha kunakuwepo mijadala mizuri zaidi.
Sitta alisema anaamini kuwa mijadala mingi itapata ufumbuzi ndani ya
Kamati zenyewe na Bunge litapokea mawazo ambayo tayari yameshafanyiwa
kazi kutokana na michango ya wajumbe.
Alipoulizwa kama ataweza kuendesha Bunge hilo bila kuyumbishwa na
shinikizo kutoka katika chama chake na vyama vingine vya siasa, alisema
kamwe atasimamia haki na hataegemea upande wa chama chake.
"Kamwe siwezi kufanya hivyo kwani kanuni zinazoendesha Bunge Maalumu
haziniruhusu kushiriki katika vikao vya chama changu cha CCM hasa
ninapokuwa nimechaguliwa kuongoza chombo hiki kama Mwenyekiti wa Bunge,"
alisema.
Alisema pamoja na kuwa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), atajitahidi kusimamia mijadala yote kwa ufasaha zaidi.
"Sasa CCM sijui wataniletea hizo hoja kwa njia ganiÉila ikumbukwe kuwa
kinachoshindanishwa si masuala ya uchama, bali ni masuala ya msingi
ambayo ni kwa maslahi ya Taifa kwa watu wote," alisisitiza Sitta.
Alipoulizwa kuhusu namna atakavyosimamia mgawanyiko uliojitokeza juu ya
kura ya siri na wazi, Sitta alisema atatumia Kamati ya Maridhiano na
Kamati ya Uongozi kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Alisema anaamini kuwa wiki hii kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda,
Pandu Ameir Kificho, itakutana kujadili suala hilo na kupata ufumbuzi.
Sitta ambaye ni mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea katika
uchaguzi huo wa Mwenyekiti, alisema anaamini busara ya kamati hiyo
italiwezesha Bunge kupata muafaka wa jambo hilo.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wake kama hautaathiri kuongoza kiti hicho,
Sitta alikiri kuwa anaamini katika serikali mbili kwa vile wanaotaka
serikali tatu wanataka kupanua wigo tu wa kujipatia madaraka.
Kampeni za Sitta kuwania nafasi hiyo zilianza muda kidogo baada ya Bunge
la Katiba kuanza ambapo wapambe wake walikuwa wakishindana na wapambe
wa aliyekuwa mshindani mkubwa ndani ya CCM, Mwanasheria Mkuu wa zamani,
Andrew Chenge.
Wakati wapambe hao wakipiga kampeni, Sitta alijitokeza hadharani na
kuelezea nia yake ambapo baada ya muda, wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya
wabunge wa CCM, waliafiki Sitta kuwa mgombea wa nafasi hiyo kutoka
katika chama hicho, huku Chenge akiondoa jina kwa hiari yake.
Jana kulisambazwa kipeperushi cha Sitta cha kuomba kura ambapo katika
mtazamo binafsi wa Silla, ilisomeka: "Ni mpenda demokrasia, mtetezi wa
haki na maslahi ya anaowaongoza, mzalendo asiyetumia vibaya madaraka
anayokabidhiwa, mtetezi wa maendeleo ya wanawake, wanyonge, walemavu;
asiyependa ubaguzi wa aina yoyote.
Dira iliyoandikwa katika kipeperushi hicho inasomeka: "Bunge la Katiba
lenye mjadala wa kushindanisha hoja kwa hoja, kwa maslahi ya Taifa, ili
kuwaletea Watanzania ndani ya muda, Katiba maridhawa inayokidhi
matarajio ya wengi na inayojenga matumaini yao ya utawala bora na
maendeleo endelevu kwa wote.
Bunge Maalumu la Katiba leo watapiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Bunge
hilo atakayeongoza hadi kumalizika kwa Bunge na kupatikana kwa Katiba
itakayopelekwa kwa wananchi kuipigia kura.
Akitangaza utaratibu wa uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge
Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho alisema fomu zimeanza kutolewa
jana kwenye ofisi ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa
Baraza la Wawakilishi ambapo mwisho ni leo saa 4:00 asubuhi na saa
10:00 jioni kutafanyika uchaguzi.
Alisema fomu kwa ajili ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti zitatolewa baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti.
"Nafasi ya Makamu Mwenyekiti itasubiri apatikane Mwenyekiti, ili
tuzingatie jinsia kama ilivyo kwenye makubaliano lakini pia kujua
Mwenyekiti ametoka upande gani wa Muungano, ili Makamu atoke upande wa
pili kama sheria inavyoagiza," alisema.
Post a Comment