Aliyekuwa mshindani wa Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi wa Jimbo la Chalinze mwaka 2000 kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (Cuf), Fabian Leonard atapambana na mtoto wa rais huyo, Ridhiwani Kikwete katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utakaofanyika Aprili 6, mwaka huu.
Chama hicho, kikimtangaza mgombea huyo Makao Makuu
ya Cuf yaliyopo Buguruni Dar es Salaam jana, kilisema kinakwenda
kulichukua jimbo hilo kutokana na wananchi wake kuendelea kuishi maisha
magumu wakati rais wa nchi anatokea jimbo hilo.
Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi iliyobaki
wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo, Said Bwanamdogo kufariki
dunia. Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdul
Kambaya akimtambulisha mgombea huyo alisema, Leonard alipambana na Rais
Kikwete mwaka 2000 wakati huo Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.
“Huyu Leonard ni mzaliwa wa Chalinze anayajua
matatizo ya wanachalinze, alipambana na Rais Kikwete lakini kutokana na
sababu mbalimbali alishindwa, sasa ni zamu yake kumpambana na
mwana,”alisema Kambaya
Leonard alisema, jimbo hilo limekuwa nyuma
kimaendeleo huku likiwa na kiongozi wa nchi ndani yake, hivyo endapo
baba alishindwa hata mtoto naye hataweza. Alisema Mkoa wa Pwani katika
matokeo ya kidato cha Nne mwaka jana imekuwa ya tatu kutoka mwisho,
huduma za afya duni na barabara hazifai. “Nimejipanga, nilipambana na
baba yake sasa kama napambana na mtoto ni dhahiri ushindi upo
hadharani”alisema Leonard.
Post a Comment