Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tumepokea amri ya Mahakama Kuu
(Kitengo cha Kazi) kukamata sh. milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana
na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji
wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.
Tayari
tumeanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo katika mechi ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa Machi 22 mwaka huu
mjini Tabora tumezuia sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa mgawo wa
Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya sh. 38,655,000.
Wachezaji
hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa
bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi na Ndlovu walishinda kesi
hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106.
Tunawakumbusha
wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu, vyama vya mpira wa miguu vya mikoa
na vyama shiriki) kuzingatia mikataba wanayoingia na watendaji wao
wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine.
Iwapo
wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate taratibu kwa vile hakuna
mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande mmoja unataka
kufanya hivyo.
*AZAM, YANGA VIWANJANI DAR, TANGA VPL
Timu
za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara zinashuka tena viwanjani
kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania pointi tatu.
Azam
yenye pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi
itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mgambo Shooting ipo
katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL ikiwa na pointi 19.
Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na
Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga ipo nyuma ya Azam kwenye
msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47. Hata hivyo, timu hiyo ina
mchezo mmoja mkononi.
Tanzania
Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David Mwamaja hivi sasa ina pointi 22
ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za mwisho katika ligi hiyo
itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi Ligi Daraja la
Kwanza (FDL).
Ligi
itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ashanti
United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo
Chamazi, Dar es Salaam.
Jumapili
(Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Tanzania
Prisons (Uwanja wa Sokoine), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Uwanja wa
Kaitaba), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu), JKT Ruvu na
Rhino Rangers (Uwanja wa Azam Complex), Azam na Simba (Uwanja wa Taifa)
na Mgambo Shooting na Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).
*KAMATI YA SHERIA KUPITIA MAREKEBISHO YA KATIBA
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) inatarajia kukutana mwishoni mwa wiki kupitia taarifa ya
utekelezaji wa agizo la wanachama kurekebisha katiba zao.
TFF
tulitoa agizo kwa wanachama wetu kufanyia marekebisho katiba ikiwemo
kuingiza Kamati ya Maadili. Mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo ulikuwa
Machi 20 mwaka huu.
Hivyo,
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itapokea taarifa ya utekelezaji
wa agizo hilo kutoka kwa Sekretarieti, na baadaye kutoa mwongozo wa
hatua inayofuata.
*TIMU YA WATOTO WA MITAANI YAENDA BRAZIL
Timu
ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza imeondoka leo
(Machi 26 mwaka huu) kwenda Brazil kushiriki mashindano ya Kombe la
Dunia kwa Watoto wa Mitaani.
John
Kadutu ambaye ni mjumbe wa Bodi ya kituo hicho, na pia mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha
klabu za Mkoa wa Mwanza ndiye kiongozi wa msafara wa timu hiyo ya
Tanzania.
Michuano
hiyo ya siku 10 inayoshirikisha watoto wa mitaa (wavulana na wasichana)
inaanza keshokutwa (Machi 28 mwaka huu). Nchi 19 zinashiriki michuano
hiyo itakayofanyika katika Jiji la Rio de Janeiro.
Mbali
ya Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kwa upande wa
wavulana ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani,
Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El
Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na
Zimbabwe.
Mwaka 2010 mashindano hayo yalifanyika Durban, Afrika Kusini ambapo pia Tanzania ilishiriki.
*MABINGWA WA MIKOA WATAKIWA MACHI 30
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linavikumbusha vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa kuwa vinatakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao
kufikia Machi 30 mwaka huu.
Majina
ya mabingwa yanatakiwa kuwasilishwa pamoja na usajili wa wachezaji
waliotumika kwenye ligi ya mkoa. Kila klabu inaruhusiwa kuongeza
wachezaji watano kutoka ndani ya mkoa husika, ambapo unatakiwa
uthibitisho wa usajili huo.
Mpaka
sasa ni vyama viwili tu ndivyo vimeshawasilisha mabingwa wao. Vyama
hivyo ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ambapo bingwa
wake ni Kiluvya United, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi
(LIREFA) ambapo bingwa ni Kariakoo SC.
Post a Comment