Mambo
yanazidi kuwa matamu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Kalenga, Iringa Vijijini, ambapo leo asubuhi helkopta ya Chadema
iliuteka mji wa Iringa kwa kurusha vipeperushi vya mgombea wao Grace
Tendega, katika maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa hasa katika stendi
kuu ya mabasi na zingine zilitua Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Iringa.
Kwa mujibu wa shuhuda ambaye ofisi yake
ipo mkabala na Ofisi za CCM, alisema kuwa majira ya saa nne leo asubuhi
waliona helkopta ya Chadema ikipita kwa chini karibu na majengo huku
ikidondosha vipeperushi katika maeneo hayo.
"Mimi na wenzangu tulishituka na
kutoka nje kuiona helkopta hiyo, kwanza tulidhani inatua lakini haikuwa
hivyo. tuliona ikirusha vipeperushi ambavyo vingine vilitua jengo la
CCM, baada ya hapo ikapaa zaidi angani na kuelekea upande wa kusini mwa
Mji wa Iringa," alisema dada huyo.
Chadema ilitangaza kwamba leo
inaanza kampeni katika Jimbo la Kalenga kwa kutumia helkopta maarufu
kama Chopa, na wangeanzia Kijiji cha Wangama alikozaliwa mgombea wao
Grace Tendega.
Post a Comment