Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
*********
Mabilioni ya shilingi yaliyowekwa na Watanzania katika benki za Uswisi yameanza kuhamishwa kimyakimya.
Ripoti ya
Benki za Uswisi ya 2012 inaonyesha kuwa fedha zinazotoka Tanzania
zimepungua kwa karibu Sh.36.4 bilioni ikilinganishwa na zilizokuwapo
2011 nchini humo, lakini haielezi sababu ya kupungua kwake.
Taarifa
za kuhamishwa kimyakimya kwa fedha hizo ambazo zinaaminika kuwekwa na
Watanzania waliowahi kuwa katika utumishi wa umma, imekuja wakati ambao
Serikali inasubiriwa kutoa taarifa yake kuhusu vigogo walioficha fedha
nchini humo, ambazo zinaaminika walizipata kwa njia zisizo halali.
Awali,
kiasi cha fedha kilichotajwa kufichwa katika benki hizo ni Sh.327.9
bilioni (Dola za Marekani 204.96 milioni), lakini taarifa mpya ya 2012
inaonyesha kuwa kiasi hicho kimepungua hadi Dola za Marekani 182.2
milioni (Sh.291.5 bilioni).
Kiasi
hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa
kilomita 300 ambao ni sawa na kutoka Morogoro hadi Iringa.
Akizungumzia
ripoti hiyo, Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema: "Hadi
mwisho wa 2012, fedha zilizopo kutoka Tanzania zimebaki Faranga za
Uswisi 160 milioni (Dola za Marekani 182.2 milioni) na siyo zile za
awali ambazo ni Faranga za Uswisi 180 milioni (Dola za Marekani 327.9
milioni)....... hivyo ndiyo kusema kuwa fedha hizo zinapungua," alisema
Chave na kuongeza:
"Inawezekana
ni kutokana na kelele za vyombo vya habari hasa Mwananchi, pengine
wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye benki za nchi nyingine. Sisi
Serikali ya Uswisi tunapochapisha ripoti kama hizi kuonyesha jumla ya
fedha kwa nchi zote duniani, haimaanishi kuwa fedha zote hizo ni
haramu."
Alisema
ni makosa kwa vyombo vya habari kuendelea kuonyesha kwamba ni Uswisi
pekee kunakofichwa fedha chafu, kwani zipo nchi nyingine ambako watu wa
mataifa mbalimbali huweka fedha zao ambazo zimepatikana kwa njia haramu.
Benki za
Uswisi zimekuwa zikidaiwa kutumika kuficha fedha chafu kutoka maeneo
mbalimbali duniani kutokana na usiri wake katika kutunza taarifa za
wateja.
Ripoti
hiyo inaonyesha kuwa Kenya inaongoza kwa nchi za Afrika Mashariki kwa
kuwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni karibu Sh.1.6 trilioni
ikifuatiwa na Uganda Sh.376.7 bilioni, kisha Tanzania Sh.291.5 bilioni.
Rwanda ina Sh.55.1 bilioni na Burundi Sh.42.2 bilioni.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alipoulizwa jana kuhusiana na
taarifa hizo mpya alisema suala hilo la fedha zilizopo Uswisi si la
kuzungumza kwenye vyombo vya habari.
"Hili
jambo ni jambo nyeti sana kwa sababu kazi tuliyopewa kuchunguza suala
hili bado hatujamaliza, kwa hiyo kuanza kulizungumza kwenye vyombo vya
habari kunaweza kuathiri kazi hii," alisema Jaji Werema.
Aliwaomba Watanzania kuvuta subira juu ya jambo hilo akisema kamati yake inaendelea kufuatilia na taarifa itawasilishwa.
Chanzo:mwananchi
Post a Comment