Mtalii kutoka
nchini Ujerumani anayefahamika kama Bi. Jeanne Traska (32) akiwa na
muongoza wageni Athuman Juma leo majira ya saa mbili na nusu asubui
wamekwama katika kilele cha Mawenzi Mlimani Kilimanjaro kwa kamba
iliyonasa na kuwafanya wasiweze kushuka chini wala kwenda juu.
Bi. Jeanne na Athuman
Juma walianza kupanda mlima kupitia Kampuni ya Nordic Tours tarehe
18.3.2014 kwa kutumia njia ya Rongai – Kibo –Marangu safari ambayo
ingewachukua siku tano. Hadi sasa taarifa za awali zinaonyesha kuwa Bi.
Jeanne alitakiwa kwenda kileleni Kibo lakini katika mazingira
yasiyofahamika alibadili uamuzi na kuelekea kilele cha Mawenzi ambacho
huwa hakitumiwi na watalii isipokuwa kwa kujaza fomu maalum inayoonyesha
kuwa mgeni amekubali kwa hiyari yake kupanda kilele hicho.
Shirika
la Hifadhi za Taifa kwa kushirikiana na Kampuni ya Nordic Tours
wanaendelea na jitihada za uokoaji kwa kutumia askari ambao wanaelekea
eneo la tukio pamoja na helikopta itakayosaidia zoezi la uokoaji kwa
kutegemea na hali ya hewa itakavyotulia ambapo hivi sasa kuna mawingu
mazito katika eneo la mlima.
Umma utaendelea kufahamishwa maendeleo ya jitihada za uokoaji kadri zitakavyopatikana.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
22.03.2014
Post a Comment