Kiongozi
wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (Wapili Kushoto) akipata maelezo ya
maendeleo ya Mradi wa Maji ya Mtiririko Kijiji cha Igurusi kutoka kwa
Mshauri wa Mradi huo Mhandisi Kimambo.
Mafundi
wakiendelea na kazi ya ujenzi huku wakaguzi hao wakikagua. Tanki hilo
lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita laki tano ambalo limeshakamilika kwa
asilimia 90. Hadi kukamilika kwake Mradi utagharimu jumla ya Shilingi
zaidi ya Milioni 830.
Naibu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (Uchumi Jumla), Prof. Longinus
Rutasitara (Aliyenyanyua Mkono) akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa
Mradi wa Maji wa Iwalanje wakati Timu ya Ukaguzi ilipotembelea Mradi
huo.
Kiongozi
wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (Mwenye nguo nyeusi) akionja maji kutoka
moja ya njia za kusambazia maji ya Mradi wa Maji wa Iwalanje. Kukamilika
kwa Mradi huo kumetoa suluhisho la adha ya muda mrefu iliyokuwa
ikiwakabili wakazi wa Kijiji cha Iwalanje na Taasisi mbalimbali za
Serikali zinazohudumiwa na Mradi huo.
Picha zote na Saidi Mkabakuli
Na Saidi Mkabakuli
Wakazi
wa mkoa wa Mbeya na vitongoji vyake wameanza kufaidi matunda ya
uwekezaji wa kimkakati uliobainishwa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011 – 2016) kupitia ujenzi wa miundombinu ya maji, ujenzi wa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, pamoja na ujenzi wa jengo la
Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Rufaa iliyopo mkoani humo.
Hayo
yalibainika wakati Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara ya ukaguzi wa baadhi miradi ya
maendeleo kushuhudia hali ya utekelezaji wa miradi iliyopo mkoani humo.
Akizungumza
wakati wa ukaguzi huo mmoja wa Kiongozi wa Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri
anayeshughulikia Huduma za Jamii na Maendeleo ya Idadi ya Watu, alisema
kuwa katika kutambua changamoto zinazowakabili wakazi wa mkoa huo,
Mpango wa Maendeleo uliweka bayana uanzishaji na uendelezaji miradi ya
maendeleo ili kutoa huduma za kijamii kwa Watanzania wote.
“Mpango
wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja
wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa
utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na
tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa ikiwemo miradi hii tunayokagua
leo,” alisema Bibi Mwanri.
Bibi
Mwanri aliongeza kuwa kwa kutambua changamoto za uhitaji wa maji kwa
baadhi wakazi wa vijijini wa mkoa wa Mbeya, Serikali iliwekeza zaidi ya
bilioni moja kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya maji ya Mradi wa
Maji ya Mtiririko Kijiji cha Igurusi na Mradi wa Maji wa Iwalanje.
“Hii
ni baadhi ya miradi inayonufaisha wakazi wa mkoa huu ambayo
tumetembelea. Kukamilika kwa Miradi hii kumetoa suluhisho la adha ya
muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Mbeya na vitongoji vyake
pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohudumiwa na Miradi hii,”
alisema.
Naye
Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara ambaye
alikuwa kiongozi mwenza wa ukaguzi huo, alisema kuwa maendeleo ya miradi
hiyo ni ishara tosha kuwa wakazi wa Mbeya na vitongoji vyake wataanza
kuneemeka na uwekezaji huo wa Serikali kwa kupata fursa mbalimbali za
kimaendeleo kupitia miradi hio.
Akitolea
mfano wa uwekezaji katika Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Songwe, Prof. Rutasitara alisema kuwa kukamilika kwa Uwanja huo ambao
umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 70, sio tu kutaongeza shughuli za
kiuchumi mkoani Mbeya bali kunatoa fursa za kufungulia za kuwezesha
ukuaji mpana wa uchumi wa nchi.
“Uwanja
wa Songwe unatoa fursa za misingi wa uchumi kwa watu walio wengi, hizi
ni juhudi za makusudi za Serikali za kuondoa vikwazo vilivyopo hivi sasa
katika kutumia utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo mkoani Mbeya,”
alisema Prof. Rutasitara.
Serikali
imeaandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukiwa na lengo la kuwa na
mfumo madhubuti wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Mpango
huu utadumu kwa mwaka 2011/12 – 2015/16 na utakuwa wa kwanza katika
mfululizo wa mipango mitatu itakayotekelezwa kwa awamu. Lengo la Dira
ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Post a Comment