Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Kebwe akihutubia kwa niaba ya
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Garib Bilal aliyekuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa kituo hicho.
Ofisa Rasilimali Watu na Utawala wa Bohari ya Dawa (MSD), Shangwe Stephen akiwa kwenye hafla hiyo.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Kebwe akiangalia maboksi ya dawa kwenye gari ambazo zilikuwa zikipelekwa
kusambazwa baada ya kuzinduliwa kituo hicho. Wanaoshuhudia kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Cosmas Mwaifwani
Mbunge wa Muleba Kaskazini,
Profesa Anna Tibaijuka. (kulia), akiteta jambo na Meneja wa MSD, Kanda
ya Mwanza ambaye pia anahudumia kituo hicho cha Muleba, Dyekwifo Sabura.
Wananchi mbalimbali wa wilayani Mulena na mkoa wa Kagera wakiwa katika hafla hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Muleba
SERIKALI imeipongeza Bohari ya
Dawa (MSD) kwa kuanzisha utaratibu wa kuweka alama ya GOT katika dawa
inazosambaza jambo litakalo saidia dawa za serikali kutambulika kirahisi
kwa wananchi hivyo kupunguza vitendo vya wizi.
Pongezi hizo zilitolewa na Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Kebwe kwa niaba ya Makamu
wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilali ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
uzinduzi wa Kituo cha Usambazaji dawa cha MSD wilayani Muleba mkoani
Kagera kilicho zinduliwa mwishoni mwa wiki.
“Naamini utaratibu huu wa kuweka
alama hiyo umeanza kufanyika hivyo naagiza utekelezwe haraka na dawa
zote ziwekewe alama hiyo ili kuepusha upotevu wa dawa za Serikali”
alisema Kebwe.
Kebwe alisema Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa imekuwa na
ushirikiano mzuri na wadau mbalimbali wa maendeleo kama vile; Mfuko wa
Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund)
na Shirika la Misaada la Maendeleo la Marekani (USAID) ambao tayari
wamekwishatoa msaada mkubwa wa ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia
dawa katika mikoa mbalimbali nchini.
Waziri Kebwe alitoa ushauri
ushirikiano huo uendelezwe ili wadau hao waweze pia kutoa msaada wa
ujenzi wa ghala la kisasa katika Halmashauri ya Muleba la kuhifadhia
dawa na vifaa tiba.
Alisema ufunguzi wa kituo hicho
cha kusambazia dawa mkoani Kagera, ni mchango tosha katika kutekeleza
Malengo ya Milenia hususan, kupunguza vifo vya akina mama na watoto, na
kupambana na UKIMWI na Malaria.
” Kituo hiki kitatumika kuongeza
ufanisi wa mfumo kufikisha dawa karibu na wananchi na kwa wakati ili
kufanikisha lengo hilo mahsusi” alisema Dk. Kebwe.
Alisema Serikali ilianzisha Bohari
ya Dawa ili kufanikisha majukumu ya kununua, kuhifadhi na kusambaza
dawa na vifaa tiba katika vituo vya umma vya kutolea huduma ya afya hapa
nchini.
Aliongeza kuwa pamoja na juhudi
kubwa ambazo Serikali inafanya kupitia MSD ili kufanikisha upatikanaji
endelevu wa dawa na vifaa tiba, bado vituo vingi vya kutolea huduma ya
afya hasa vijijini vimekuwa na tatizo sugu la uhaba wa dawa muhimu hivyo
Serikali itaendeleza juhudi hizo ili tatizo hilo liweze kupungua au
kudhibitiwa kabisa.
Alisema kwa sasa Bohari ya Dawa
inawajibika kufikisha dawa na vifaa tiba moja kwa moja hadi kituo husika
cha huduma ya afya badala ya kuishia kwa Mganga Mkuu wa Wilaya kama
ilivyokuwa hapo awali.
Kebwe alisema mfumo huu wa
ufikishaji dawa moja kwa moja hadi katika vituo vya huduma na hospitali
kwa kiasi kikubwa umesaidia sana upatikanaji wa dawa katika vituo vya
umma vya kutolea huduma ya afya hasa vijijini.
“Naagiza kuwepo ushirikiano wa
karibu kati ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (kupitia Bohari ya
Dawa) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (kupitia Ofisi
ya Waziri Mkuu) ili kuhakikisha ufanisi katika jambo hili” alisema
Kebwe.
Katika hatua nyingine Dk. Kebwe
amesema anatambua tatizo la dawa na vifaa tiba vya Serikali kupatikana
katika maduka ya dawa ya watu binafsi jambo linaloikera sana Serikali
hivyo ameiagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na
Jeshi la Polisi kufanya msako endelevu ili kuwafichua na kuwachukulia
hatua za kisheria wale wote watakaopatikana na dawa za Serikali kinyume
cha Sheria.
Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini
(MSD), Profesa Idris Mtulia alisema mkakati wa kushirikisha sekta
binafsi ili kufanikisha upatikanaji wa dawa pindi Bohari ya Dawa
inapokuwa na upungufu, unaendelea kutekelezwa sanjari na halmashauri
zote nchini kuhimizwa kununua dawa kutoka MSD kwa kutumia vyanzo vingine
vya fedha (kama vile Basket Fund, NHIF, Tele kwa Tele)
Alisema pamoja na changamoto
mbalimbali inazokabiliana nazo, Bohari ya Dawa kwa kushirikiana na
Serikali na wadau wengine, itaendelea kutoa huduma bora na kuhakikisha
kuwa dawa zenye ubora na bei nafuu zinakuwepo wakati wote kwa manufaa ya
Watanzania.
Post a Comment