MTANDAO wa Wanawake na Katiba wenye mashirika zaidi ya 50 yanayotetea haki za wanawake katika Katiba mpya, umelipongeza mchakato
na matokeo ya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa Bunge Maalum la Katiba
(Mwenyekiti na Makamu wake) ambao umezingatia usawa wa jinsia.
Kauli hiyo imetolewa leo kwa vyombo vya habari na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji, Lilian Liundi wa TGNP Mtandao kwa niaba ya Mtandao
wa Wanawake na Katiba jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa licha ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Mwaka 2012 haikuanisha kuwa
uchaguzi wa uongozi wa Bunge hili uzingatie usawa wa jinsia bunge hilo
limeona umuhimu huo.
“…Tumetambua
busara na hekima za wajumbe za kuonyesha nia ya kujenga msingi wa usawa
wa jinsia katika uongozi na vyombo vya maamuzi nchini. Kwetu sisi, hili
si suala la uwepo wa mwanamume na mwanamke katika uenyeketi wa Bunge
Maalumu tu, bali pia ni ukomavu wa kipekee wa wajumbe katika kuuona
ukweli kuwa suala la kuimarisha sauti za wanawake na wanaume ni nyeti
sana, haswa wakati wa ujenzi wa maridhiano muhimu kikatiba,” alisema Liundi.
“Tunawapongeza waliochaguliwa ambao ni Mhe. Samweli Sitta (Mwenyekiti) na Mhe. Samia Hassan Suluhu (Makamu Mwenyekiti) kwa kuaminiwa katika nyadhifa hizo muhimu. Mtandao
wa Wanawake na Katiba unatambua uwezo wao katika utendaji na una
matumaini makubwa kuwa pamoja na mengine mengi watakayoyasimamia,
watatoa uongozi ulio imara na wenye weledi wakati wakiongoza Bunge hili
katika kujadili na kupitisha misingi muhimu itakoyopelekea katika ujenzi
wa usawa wa kijinsia nchini.”
Alisema mtandao huo unategemea
kuona usawa wa jinsia ndani ya Katiba mpya, ambao sio ule tu wa
kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali, lakini pia usawa
ulio na nia ya kujenga misingi ya kuleta maendeleo ya kweli kwa
wananchi walio wengi na haswa wanawake nchini.
“…Kwa
mtazamo huu, tunatarajia kuwa busara za Wenyeviti hawa na washauri wao
zitatumika pia kuzingatia usawa wa kijinsia katika Kamati zitakozoundwa
pamoja na kuwa kuzingatia ustadi na uzoefu wa wanakamati unahitajika.
Nia kubwa ikiwa kuona wanawake kwa wanaume watatoa sauti zao kuhakikisha
na kulinda, pamoja na mengine, uzingatiwaji wa usawa wa jjinsia katika
vifungu vyote vya Katiba mpya.”
Aidha alifafanua kuwa Mtandao
wa Wanawake na Katiba, unawapongeza wajumbe wote wanawake kwa umoja
wao, mshikamano na ushirikiano imara, ambao umeleta mafanikio makubwa
katika michakato inayoendelea huko Dodoma kwenye Bunge Maalumu.
“…Huu
ni mwanzo wenye kuonyesha mifano mizuri, na ambao tunapenda kuuona
ukiendelezwa na kusimamiwa imara wakati wote Bunge Maalumu litakapokuwa
likifanya kazi yake ya kuchambua na kupitisha vifungu mbalimbali vya
Katiba,” alimalizia Bi. Liundi
Post a Comment