Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu
mfumuko wa bei nchini.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa
hali ya mfumuko wa bei nchini imeendelea kuwa katika kiwango
kisichobadilika katika kipindi cha mwezi Januari na Februari mwaka huu
kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma
mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na
Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa
mwezi Februari 2014 umeendelea kubaki katika kiwango cha asilimia 6.0
kama ilivyokuwa mwezi Januari mwaka huu.
Amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei za
bidhaa na huduma kwa mwezi Februari 2014 imebakia kuwa sawa na ile
iliyokuwepo mwezi Januari huku kukiwa na ongezeko dogo la upandaji wa
bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma mwezi kwa mwezi Februari 2014
ikilinganishwa na bei za mwezi Februari mwaka jana.
Ameeleza kuwa mfumuko wa bei za bidhaa
za vyakula na migahawa kwa mwezi Februari umeongezeka hadi asilimia 6.9
kutoka asilimia 6.6 za mwezi Januari mwaka huu huku bidhaa zisizo za
vyakula kasi ya ongezeko la bei ikipungua hadi asilimia 6.3 mwezi
Februari 2014 kutoka asilimia 6.7 za mwezi Januari mwaka jana.
Amefafanua kuwa mwenendo wa bei za
bidhaa za vyakula kama samaki, mbogamboga, ulezi na matunda zimeonyesha
kuongezeka kwa kiwanga kikubwa kwa mwezi Februar ikilinganishwa na bei
za bidhaa hizo kwa mwaka uliopita huku bei za bidhaa zisizo za vyakula
za vitambaa vya suti za wanaume, kodi za pango la kuishi, mkaa, na nauli
za bajaji zikionyesha ongezeko.
Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa
kwa kipimo cha mwezi,ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kwa asilimia 1.4
ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.8 kwa Januari mwaka huu, huku
fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 148.62 kati ya
Februari mwaka uliopita na Februari mwaka huu.
Amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko
la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na dagaa,samaki wakavu,
mbogamboga na viazi mviringo huku bidha zisizo za vyakula zikiwa pombe
za kienyeji, vitambaavya suruali, viatu vya wazi vya plastic, mafuta ya
dizeli na Petroli pamoja na huduma za unyoaji na usafi wa nywele.
Aidha kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa
bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Februari umeonyesha
kupungua na kufikia shilingi 67 na senti 29.
“Kupungua kwa thamani ya Shilingi
kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa
Shilingi 100 mwaka jana, basi kwa mwaka huu itampasa aongeze zaidi ili
aweze kununua kitu kama kile kile, kwa mfano badala ya shilingi 100
inabidi atumie Shilingi 132”
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa
Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo
unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umepungua kidogo
na kufikia asilimia 6.86 kwa mwezi Februari kutoka asilimia 7.21 za
mwezi Januari , huku Uganda ikiwa na asilimia 6.7 kwa mwezi uliopita
kutoka asilimia 6.9 za mwezi Januari.
Post a Comment