KLABU
ya Etoile du Sahel ya Tunisia imewasilisha barua ya kurasa tatu
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ikimtaka mshambuliaji wa Yanga,
Emmanuel Okwi awalipe Dola 1.3 milioni za Kimarekani ambazo ni zaidi ya
Sh 2 bilioni za Tanzania kama fidia.
Etoile
kwenye barua hiyo ambayo Mwanaspoti ina nakala yake, imewasilishwa Fifa
na klabu hiyo inataka ilipwe fedha hizo za fidia baada ya mchezaji huyo
kuvunja mkataba wake na klabu hiyo kinyume na sheria za Fifa na wakaenda
mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa mchezaji huyo kuna watu walimrubuni.
Gharama
hizo ni pamoja na fidia za uhamisho, mshahara wa Juni mwaka jana,
mshahara wa kuanzia Julai mwaka jana hadi Juni 2016, posho zake za
kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2016, gharama za malazi, gharama za tiketi
ya ndege, gharama za usafiri wa gari, mshahara wa miezi mitano
aliolipwa, pamoja na gharama za kiinua mgongo baada ya kumaliza mkataba
na Etoile.
Barua
hiyo ambayo Katibu Mkuu wa Etoile, Adel Ghith aliipeleka Fifa kama
utetezi wao kwenye kesi dhidi ya Simba na Okwi, pia aliitoa kwa Simba
ikionyesha kuwa Okwi anatakiwa kuilipa Etoile zaidi ya billioni mbili za
Kitanzania.
Ghith
alisema: “Ni tabia mbaya iliyofanywa na Okwi ambayo haiwezi kuvumilika
na hivyo ninaomba Fifa mtupe muongozo kwani mchezaji huyo amevunja
mkataba bila kufuata utaratibu na kwa njia isiyokubalika kisheria, tena
tunaomba fidia ya gharama kama ifuatavyo.
“Fidia ya
gharama za usajili Dola 247, 142 (sawa na Sh 393.6 milioni ),mshahara
wa Mei hadi Juni 2013 ambao ni Dola 10,000 (sawa na Sh 15.9
milioni),mshahara wa Julai 2013 hadi Juni 2016 ambazo ni Dola 180,000
(Sawa na Tsh 293 milioni) na posho Dola 480,000 (sawa na Sh 764.5
milioni) kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2016.
“Gharama
nyingine ni kodi ya miezi 38 ambayo ni Dola 19,000 (sawa na Sh 30.2
milioni), tiketi za ndege za Dola 12,000 (sawa na Sh 19.1 milioni),
usafiri wa ndani (gari) Dola 26,600 (sawa na Sh 42.3 milioni), mshahara
uliolipwa kwa miezi mitano ya awali Dola 50,000 (sawa na Sh 79.6
milioni), pamoja na kiinua mgongo ambacho angepewa baada ya kumaliza
mkataba na Etoile cha Dola 300,000 (sawa na Sh 477.8 milioni),”
alieleza.
Barua
hiyo ya Etoile imeambatanishwa na nakala sita za muhimu ambazo ni
mkataba wa Okwi na Etoile, maelezo ya Fufa (Shirikisho la Soka Uganda),
nakala ya ratiba za mazoezi na michezo ya klabu, nakala iliyotafsiriwa
kwa Kiingereza yenye ratiba za mazoezi na michezo ya klabu hiyo, barua
ya mchezaji ya kujiunga na klabu pamoja na Leseni ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) ya mchezaji.
Ghith
alieleza kwenye barua hiyo kuwa: “Tulifurahi kuona Okwi akifanya kazi
yake vizuri, alifanya hivyo mwanzoni kabla ya kubadilika lakini alikuwa
akishiriki shughuli zote za timu ikiwemo hata kukichezea kikosi cha U-23
cha klabu hiyo.
“Alikuwa
akilipwa mshahara wake kwa kipindi chote alipokuwa na timu na hivyo
alikuwa akilipwa kwa mujibu wa taratibu za Fifa na zile za Shirikisho la
Soka Tunisia,” alisema Ghith kwenye barua hiyo.
Ghith
katika barua hiyo pia alisema: “Ghafla mwezi Mei Okwi alibadilika na
hata kushindwa kuhudhuria na kujiunga na timu. Alianza kukosa mazoezi
lakini bado tulipeleka jina lake kwa ajili ya mashindano ya Shirikisho
Afrika lakini baadaye aliondolewa.
“Baada ya
kuwa hivyo, alipoacha kucheza kuna malipo alikuwa akilipwa kama
mchezaji wetu lakini kuna mengine tulisitisha na tukamwambia kuwa
hatutaweza kumlipa kutokana na sheria za Shirikisho la Soka la Tunisia
kwamba mchezaji atalipwa baadhi ya malipo pale tu anaposhiriki mchezo
“Tulipokea
barua ya Fufa kumualika Okwi kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la
Dunia Brazil 2014 dhidi ya Liberia na Angola, michezo ambayo iliandikwa
kwenye barua kuwa ingeanza tarehe 8-15 Juni 2013 lakini tuligundua kuwa
Mei 20, 2013 Okwi tayari alikuwa Uganda bila ruksa maalumu wala
makubaliano yoyote na klabu.
“Lakini
pia tuliwasiliana na shirikisho letu la Tunisia pamoja na Fufa lakini
mchezaji (Okwi) hakutaka kuwasiliana na sisi ili kumaliza matatizo.
“Tarehe
12 Julai mwaka jana, tuliwasiliana na Fufa na mchezaji ili tuje kumaliza
matatizo na pia kumwonyesha utaratibu pamoja na jinsi mkataba wake
ulivyo lakini hakutaka kusikia lolote,” alisema Ghith kwenye barua hiyo.
Ghith
alimalizia kwa kusema: “Tunadhani alishawishiwa na akaamua kuvunja
mkataba kwa njia isiyo sahihi na hivyo kutokana na matukio yote hayo
ndiyo maana tulichelewa kumlipa mshahara wake lakini pia tulimpa tu
kumpendelea kwani hakustahili kulipwa.”
SOURCE: MWANASPOTI/MWANANCHI


Post a Comment