Mwenyekiti
wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, akizungumza na
mjumbe wa Bunge hilo, SamuelSitta (kushoto), ndani ya Ukumbi wa Bunge,
Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.
Dodoma.
Siku moja baada ya kuteuliwa na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu
la Katiba, Waziri wa Ushirikiano wa AfrikaMashariki, Samuel Sitta
amesema ameanza kupitia sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza
huku akiahidi kutenda haki kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza
mjini Dodoma jana, Sitta alisema: "Nawashukuru wote waliokuwa
wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa nitatenda haki kwa wajumbe wote wa
Bunge Maalumu la Katiba."
Alisema
kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo ni kuhakikisha kuwa anazipitia
sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo na sheria nyingine kwa kuwa
ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia
mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho na mchuano uliokuwapo kati yake
na Mbunge wa Bariadi Magharibi, AndrewChenge alisema: "Hii ni hatua ya
awali na ya kawaida tu ndani ya CCM. Mara nyingi chama changu kikiona
kuna mambo yanayoleta msuguano, basi huamua kuteua jina moja kwa ajili
ya kugombea. Wameteua majina mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru
chama changu kwa kuniteua na kwa sasa najiandaa na uchaguzi."
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa
upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi ya
Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassanaliwaambia waandishi wa habari
jana kwamba ana uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na
hana shaka katika uteuzi wake.
Samia
ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),
alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo haitiliwi shaka kwa weledi
wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi hiyo.
"Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote," alisema.
Samia
aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake na baadaye, Waziri wa
Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kuwa Waziri wa
Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato.
Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta
kuwania nafasi hiyo na kusema ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya
chama.
Hata
hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake kujitoa baada ya
kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa ushauri.
Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana alisema:
"Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba, angeweza
kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili walionyesha nia;
Sitta na Chenge.
"Wote
hawa wana sifa kwa historia za maisha yao. Chenge aliwahi kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sitta, Waziri wa Sheria na Katiba,
halafu wote ni wanasheria. Hawa wote wakaanza kutafuta maoni kwa wenzao
na kila mmoja akitafuta wenzake wa kumuunga mkono. Kwa sababu wote ni
wanaCCM na kwa kuogopa makundi, tukaona tuwaite na kuwaambia jamani nyie
wote ni wetu, tusingependa mkalumbane.
"Tukawaambia
washauriane na kufikia mwafaka. Chenge akajitoa mwenyewe na jana
(juzi), kwenye mkutano, WanaCCM wote wakaamua kumuunga mkono Sitta."
Mjadala moto bungeni.
Wakati
huohuo; mjadala wa kanuni za Bunge la Katiba umeendelea kuwa moto baada
ya baadhi ya wajumbe kutaka kanuni zitambue haki ya mwanamke katika
nafasi hiyo ya juu ya uongozi.
Malumbano
hayo yalizuka wakati wajumbe hao walipokuwa wakijadili kanuni ya saba
inayohusu uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake. Mjumbe wa bunge hilo,
Christine Mzava alishauri kuwa endapo mwenyekiti atakuwa mwanamume,
makamu wake awe mwanamke.
Akijibu
hoja hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, Magdalena Rwebangila alisema kwa
kuwa sheria imetamka kuwa mwenyekiti akitoka Tanzania Bara, makamu
atatoka Zanzibar, itakuwa vigumu kuweka uwiano mwingine wa kijinsia.
Baada ya
ufafanuzi huo, Lediana Mng'ong'o alisimama na kusema: "Kwani mnaona
ugumu gani wa kuongeza hicho kipengele? Mbona Rais katika uteuzi wa
wajumbe 201 alizingatia uwiano wa kijinsia?"
Mjumbe
mwingine wa Kamati ya Kanuni, George Simbachawene alisema haiwezekani
kuwa na aina mbili za uwiano. Hali hiyo ilimfanya mjumbe mwingine, Dk
Ave-Maria Semakafu kusimama na kuomba busara itumike na kutengua kanuni
kwa kuweka nafasi sawa.
Hata hivyo, Mjumbe Ezikiah Wenje alisema itakuwa ajabu kumchagua mtu katika nafasi hizo kwa sababu tu ni mwanamke.
"Demokrasia
inahitaji ushindani sawa na hao kinamama wanaamini tuko sawa. Mimi
naomba kama kuna mtu ana sifa za kuwa mwenyekiti au makamu, wagombee
washindane," alisema.
Maelezo
hayo yaliwafanya wajumbe wanawake kusimama na kuanza kuimba: "Tunataka
haki zetu, tunataka haki zetu." Kuona hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni,
Anna Abdallah alisimama na kuwataka wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano waliopitisha sheria hiyo kujilaumu kwa sababu walipaswa
kuliangalia hilo.
Chanzo, mwananchi


Post a Comment