Umeibuka
ulevi mpya nchini ambao umethibitika kuwateka vijana hasa wa jiji la
Dar es Salaam, huku kukiwa na taarifa za kitaalamu kwamba ulevi huo una
athari za kiafya kwa watumiaji.
Ulevi huo ni kupitia starehe
au anasa mpya ya uvutaji shisha; ulevi ambao watengenezaji hutumia
chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku,
maji na moto.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti
hili umebaini kuwa tumbaku huwekwa katika chombo hicho na kuunguzwa kwa
moto, kisha moshi wa tumbaku hupita kwenye maji na huingia kwenye
bomba, kisha watumiaji huanza kuvuta.
Sehemu maarufu ambako shisha
inauzwa ni Ufukwe wa Coco, maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Sinza
Barabara ya Shekilango na maeneo kadhaa ya mitaa ya mjini.
Mmoja wa watumiaji wa shisha,
Ismail Ndunguru alisema yeye na vijana wenzake hutumia siku za mwisho wa
wiki kwenda kuburudika kwa uvutaji katika hoteli moja iliyopo mjini,
Mtaa wa Garden jijini Dar es Salaam.
“Kuvuta shisha kwa siku nzima
ni Shilingi 10,000, mkimaliza, mnarudisha bomba. Tukiwa vijana wengi
inafurahisha sana kuvuta,” alisema Ndunguru.
Taarifa za Shirika la Afya
Duniani (WHO) zinaeleza kuwa, mkupuo mmoja wa shisha, una kemikali hai
4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya
moyo na maradhi ya mfumo wa upumuaji.
WHO inaeleza kuwa, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 au 200.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya
ndani ya mwili na mfumo wa hewa, Meshack Shimwela alisema madhara ya
shisha ni kama yale yanayosababishwa na uvutaji wa sigara pengine na
zaidi kutokana na kilevi hicho kuwa na tumbaku nyingi.
Dk Shimwela alisema licha ya
kuwa watengenezaji na wavutaji wa shisha hudai kuwa haina madhara kwa
sababu huchanganywa na maji, lakini bado madhara yake ni makubwa.
“Marahi yote yanayosababishwa
na uvutaji wa sigara ndiyo yanayosababishwa na shisha, kwa mfano
saratani ya mapafu na mdomo, kifua kikuu na mzio ambao unaweza
kusababisha pumu,” alisema Dk. Shimwela.
Dk. Shimwela alisema ni vizuri
watumiaji wakajua madhara ya shisha, badala ya kuchukulia kuwa ni
mtindo wa maisha tu au starehe isiyo na madhara.
Post a Comment