Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi Meki Sadiki (kushoto) akizungumza na
mkazi wa eneo la Mloganzila Bw. Fredy Justine Masondole (kulia) ambaye
aliweka pingamizi kuzuia miundombinu ya maji, umeme na barabara kupita
katika eneo lake , Hata hivyo mkazi huyo aliruhusu ujenzi kuendelea
baada ya mazungumzo ya kupatikana kwa muafaka kufikiwa. Katikati ni
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Mhandisi Felchian Mramba.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi Meki Sadiki (katikati) akizungumza
jambo wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha
Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili(MUHAS) lililo kwenye mpaka wa
wilaya ya Kisarawe na mkoa wa Pwani leo.Wengine kutoka kushoto ni
Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi.Therezia Mmbando,Mkurugenzi
Mkuu wa DAWASA Bw. Archard Mutalemwa na Meneja wa Tanroad mkoa wa Dar es
salaam Bw. Ndyamukana Julius.
Mkazi
wa eneo la Mloganzila Bw. Fredy Justine Masondole (Katikati)
akiwapeleka katika eneo la nyumba yake lenye mgogoro viongozi wa mkoa wa
Dar es salaam wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meki
Sadiki (upande wa nyuma katikati), mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan
Lugmbana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando.
Mafundi
wakiendelea na ujenzi wa awali wa ofisi za muda katika eneo
itakapojengwa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha
Muhimbili(MUHAS) lililo kwenye mpaka wa wilaya ya Kisarawe na mkoa wa
Pwani leo
Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.
……………………………………………………………………………………………………
Na Aron Msigwa.
Baadhi
ya wakazi wa eneo la Mloganzila waliokuwa wamezuia maeneo yao kutumiwa
kupitisha miundombinu ya maji, barabara na umeme kwa ajili ya ujenzi wa
Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha
Muhimbili(MUHAS) wamekubali kuyatoa maeneo yao ili kuruhusu kuendelea
kwa ujenzi wa miundombinu hiyo.
Wakazi
hao waliozuia ujenzi huo kwa madai ya kutolipwa fidia na baadhi yao
kwenda mahakamani wamefikia uamuzi huo leo mara baada ya mazungumzo
baina yao na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi Meki Sadiki
aliyetembelea eneo la mradi huo.
Akiwa
katika eneo la ujenzi wa mradi huo unaojengwa na Kampuni ya Colon
Global Corporation kutoka Korea, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi
Meki Sadiki amesema kuwa mradi huo kwa muda umeshindwa kuendelea
kutokana na kukosekana kwa maji,umeme na miundombinu ya barabara.
Amesema
mkandarasi alikwisha onyeshwa eneo hilo la ujenzi toka Februari 23 na
kuongeza tayari makabidhiano ya eneo hilo lililo mpakani mwa wilaya ya
Kisarawe na mkoa wa Pwani yamekwishafanyika.
“Ujenzi
wa hospitali hii kubwa na chuo Kikuu cha Afya na Tiba ni moja ya ahadi
ya Rais Jakaya Kikwete, Mh. Rais aliahidi na kama mnavyoona ujenzi huu
umeanza lakini umekwamishwa na baadhi ya wananchi wachache na kama
serikali tumeona si vema tuendelee kuchelewesha ujenzi wake” Amesema.
Amesema
mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO),
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) na Wakala wa
Barabara Nchini (TANROAD) umekaa kwa pamoja ili kupata ufumbuzi wa
mgogoro huo ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa mradi huo haraka
iwezekanavyo.
“Tumekua
na mazungumzo na wenzetu hawa na leo tulikua na kikao cha pamoja ili
tupate ufumbuzi wa suala hili na tayari wakazi hawa wawili ambao nyumba
zao ziko kwenye eneo yatakapopita mabomba ya maji, nguzo za Umeme na
Barabara tumezungumza nao na tayari wamekubali na kesho ujenzi
unaendelea” Amesisitiza.
Ameongeza
kuwa wamiliki wa maeneo hayo wamekubali busara itumike kwa wao kuruhusu
mradi huo uendelee na kufafanua kuwa tathmini ya nyumba na maeneo yao
inaendelea kufanyika ili waweze kulipwa stahiki zao.
“Tumeamua
busara itumike ili kuokoa muda unaozidi kupotea na kuchelewesha ujenzi
wa mradi huu mkubwa wenye manufaa kwa wananchi,licha ya kwamba baadhi
yao wamekwishapeleka madai yao mahakamani”
Kuhusu
sehemu ya eneo la mradi huo linalomilikiwa na JWTZ, Mh. Sadiki amesema
kuwa atakwenda kuzungumza na Mamlaka husika ili kupata ufumbuzi wa jambo
hilo na kutoa wito kwa wananchi ambao tayari wamekwisha pokea fidia zao
kupisha ujenzi wa mradi huo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Mhandisi Felchian Mramba akiwa
katika eneo la tukio ameeleza shirika lake limeshindwa kufikisha umeme
katika eneo husika kutokana na zuio lililowekwa na wananchi hao na
kuongeza kuwa muafaka uliofikiwa leo ni faraja kwao kuwezesha kazi hiyo
kuendelea.
“Sisi baada ya maelewano haya ni kazi kuendelea na kesho kazi ya kupitisha nguzo na nyaya inaendelea” amesisitiza.
Mkurugenzi
Mkuu wa DAWASA Bw. Archard Mutalemwa amefafanua kuwa tayari wao kama
wahusika wakuu wa usambazaji wa miundombinu ya maji wameshalaza
miundobinu hiyo kwa 50%, kujenga mnara wa tenki kubwa la maji, kununua
vifaa na kuongeza kuwa wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa muda
uliopangwa.
Naye
Meneja wa TANROAD mkoa wa Dar es salaam Bw. Ndyamukana Julius ameeleza
kuwa ujenzi wa barabara za eneo hilo utakamilika mwezi Agosti mwaka huu.
“Sisi
tumejipanga vizuri kukamilisha ujenzi huu kwa kushirikiana na wenzetu
ili kufikia tarehe 22 Agosti mwaka huu tukamilishe kazi” Amesema.
Post a Comment