WASOMI
mbalimbali wa vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM) na Dar es Salaam (UDSM),
wametetea mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kudumisha
amani na utulivu licha ya changamoto zinazojitokeza.
Walisema
hayo walipohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana. Walisema
Muungano huo ni wa kipekee katika Bara la Afrika na duniani kwani kwa
kipindi chote cha miaka 50, utulivu, amani na mshikamano, vimedumishwa.
“Duniani
kote hali ya amani hasa kwa miaka ya hivi karibuni ni ya kutatanisha na
kutawaliwa na vurugu za maandamano ya kupinga mambo mbalimbali, zikiwemo
serikali, lakini kwa Muungano wa Tanzania, hali ni shwari na wananchi
wanaishi kwa ushirikiano na mshikamano mkubwa, ” alisema Mhadhiri wa
UDOM, ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mhadhiri huyo aliungwa mkono na wenzake wawili.
Mkuu wa
Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya UDSM, Dk Benson Bana, alisema
jambo la msingi kwa sasa ni kwa Watanzania kutafuta muafaka wa
kuendeleza umoja na mshikamano, badala ya kung’ang’ania mjadala wa mfumo
wa serikali ngapi.
Hata
hivyo, alibainisha kuwa kwa mtazamo wake, anaona mfumo bora
utakaoendeleza mshikamano kwa Watanzania na kutatua kero zote ni ule
utakaoimarisha na kudumisha Muungano.
Akizungumza
na gazeti hili Dar es Salaam jana, Dk Bana alifafanua kuwa hakuna mfumo
wowote utakaowekwa au kuchaguliwa uwe wa serikali moja, mbili au tatu,
ambao hautakosa mazuri na mapungufu bali jambo la msingi kuleta umoja na
mshikamano wa taifa.
Alisema
wakati umefika kwa Watanzania kutumia fursa hiyo ya kupata Katiba mpya
kwa kukuna vichwa na kutafuta mfumo wa serikali utakaoendana na hali
halisi ya uchumi, kisiasa na kijamii.
Kwa
mtazamo wake alisema jibu ni Serikali moja, itakayokuwa na dola moja
itakayoendeleza mshikamano na kuwaunganisha Watanzania wote wa Bara na
Zanzibar.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia
Suluhu, amesema pande zote mbili za Muungano zinafanya kila juhudi za
kuhakikisha kwamba kero za Muungano zinashughulikiwa na kupatiwa majibu
muafaka kwa majadiliano.
Alifafanua
kwamba mambo ambayo yanashughulikiwa ni pamoja na yanayohusu uchumi
ambayo kwa mipango iliyopo hivi sasa yatapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
CHANZO:HABARILEO
(MM)
Post a Comment