TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo yenye jukumu la kusimamia sekta ya Vijana nchini imeandaa
Kongamano la Vijana kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu kuhusu Wajibu wa Vijana katika
Kuimarisha Muungano Wetu Miaka 50 tangu kuzaliwa kwake.
Kongamano hili la Vijana kuhusu
Muungano linafanyika Jumapili Machi 30, 2014
kuanzia Saa 5:00 Asubuhi katika
ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam na litarushwa moja kwa moja na
Televisheni ya Taifa, TBC One na TBC Taifa.
Kongamano hili ni sehemu ya
sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tangu kuasisiwa kwake
na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume
aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Aprili 26, 1964.
Kauli mbiu ya sherehe za Miaka
50 ya Muungano ni “UTANZANIA WETU NI
MUUNGANO WETU, TUULINDE, TUUIMARISHE NA KUUDUMISHA”.
Lengo la Kongamano hili ni
kuzungumzia Wajibu wa Vijana katika kuimarisha Muungano ambao mwezi ujao
unafikisha miaka 50. Washiriki wa Kongamano
hili ni vijana 300 kutoka Vyuo vya
Elimu ya Juu vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Washiriki wa Kongamano hili watapata
fursa ya kuwasikia watoa mada ambao ni Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Prof. Gaudens Mpangala atakayewasilisha
mada kuhusu Wajibu wa Vijana katika Kuimarisha Muungano, Miaka 50 tangu
kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Aidha mada kuhusu Mapendekezo
ya Katiba Mpya kwa Mustakabali wa Muungano wetu itawasilishwa na Prof. Issa Shivji.
Waandishi wa Habari kutoka Vyombo mbali
mbali vya Habari nchini wanakaribishwa kushiriki kwa lengo la kuhabarisha umma
kuhusu kongamano hili.
Imetolewa
na Idara ya Habari - MAELEZO
29 Machi 2014
Post a Comment