Wiki
ya Machi 18 - 22, 2014 ilianza kwa siku ya Jumanne Mwenyekiti wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba
aliwaslisha rasmi Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Bunge Maalumu la Katiba. Wiki hiyo imeishia kwa siku ya Ijumaa
Rais wa Jamhuri ya Muungano ndugu Jakaya Mrisho Kikwete kutoa hotuba kwa
Bunge Maalumu. Hotuba zote zimepokelewa kwa hisia tofauti kulingana na
msimamo wa kila mtu kuhusu hoja inayoonekana ni kubwa
kuliko
zote katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya - Muundo wa Muungano. Wale
wanashabikia muundo wa Serikali Tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya
Jaji Warioba. Wale wanaoshabikia muundo wa Serikali mbili walifurahishwa
mno na hotuba ya Rais Kikwete. Sikufurahishwa na hotuba zote mbili.
Moja,
hotuba zote mbili zilichukua muda mrefu zaidi kuelezea sura moja tu ya
Rasimu ya Katiba nayo ni sura ya Sita inayohusu muundo wa Jamhuri ya
Muungano kana kwamba Katiba hii inahusu suala hilo tu. Ni dhahiri suala
hili ni kubwa na muhimu kwani linahusu uhai wa Dola yenyewe na siwezi
kubeza. Hata hivyo masuala kama Haki za Raia ni muhimu zaidi kwani hata
uwe na muundo wa namna gani wa muungano au hata muungano wenyewe
kuvunjika, bila ya kuwa na haki za msingi za raia kwenye katiba katiba
hizo zitakataliwa tu na wananchi. Huu mtindo unaozuka wa kudhani muundo
wa muungano ndio mwarobaini wa matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya
madaraka, ubadhirifu, umasikini, elimu ya hovyo, afya dhaifu,
utatufikisha pabaya na hata kurudi tena kuandika katiba kudai haki hizo.
Jaji Warioba na Rais Kikwete wameshindwa kuruka kiunzi cha kwamba
Katiba ni zaidi ya Muungano.
Pili,
wote wawili Rais Kikwete na Jaji Warioba wamejenga hoja zao kuhusu
miundo ya Muungano wanayopendekeza au kuunga mkono kutokana na misingi
ama ya 'malalamiko' au 'hofu'. Jaji Warioba aliorodhesha malalamiko 11
ya upande wa Zanzibar dhidi ya Muungano na malalamiko 10 ya upande wa
bara. Kimsingi malalamiko yote ya upande wa bara yanazaliwa na vitendo
vya upande wa Zanzibar isipokuwa lalamiko namba vii linalohusu kupotea
kwa utambulisho wa Tanganyika katika muundo wa Muungano.
Jaji Warioba anajenga msingi wa pendekezo la Tume yake kutokana na kujibu malalamiko au maarufu kero za Muungano na anasema
"....muundo
wa Serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali
mbili waliotuchia waasisi siyo uliopo sasa...... waasisi walituachia
Muungano wa Nchi Moja yenye Serikali mbili, na siyo Nchi Mbili zenye
Serikali Mbili". Nukuu hii niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee
wangu Warioba.
Rais
Kikwete alijenga msingi wa maoni yake kwenye hofu za kuwa na Serikali
tatu. Hofu hizo ni pamoja na gharama za kuendesha Muungano, kuzuka kwa
hisia za Utaifa wa Utanganyika na Uzanzibari, uwezekano wa Muungano
kuvunjika kwa kushindwa kuhudumia majeshi na hata Jeshi kuchukua Nchi
ikipidi na kutupilia mbali katiba na Serikali ya Muungano kutokuwa na
Rasilimali zake. Rais alisema 'Serikali ya Muungano ni egemezi na
tegemezi' nukuu ambayo niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee
wangu Jakaya Kikwete.
Rais
Kikwete hakuniridhisha kabisa namna ya kumaliza kero za Muungano kwa
muundo uliopo sasa kwani muundo huo umeshindwa kuzimaliza kwa takribani
miaka 50 tangu Muungano uundwe. Haiwezekani muundo uliozalisha kero
lukuki ndio utarajiwe kuzimaliza kero hizo. Kwa vyovyote vile ni lazima
kuwa na muundo mpya lakini kiukweli ni lazima muundo huo mpya ujibu hofu
alizoeleza ndugu Rais maana ni hofu za kweli.
Jaji
Warioba hakuniridhisha na namna suala la Uraia litakavyotatuliwa kwani
kutoa jibu la kubakia na 'kukubali' Nchi mbili halafu uraia mmoja
kunaleta mashaka makubwa. Kama tunataka kuwa na Uraia mmoja ni lazima
tuwe Nchi moja, hatuwezi kuwa na Nchi mbili uraia mmoja.
Vilevile
vyanzo vya mapato ya Muungano ni vidogo mno kuendesha dola. Hivyo basi
rasimu iliyopo mbele ya Bunge Maalumu ina mapungufu makubwa japo imetoa
mapendekezo yatakayomaliza malalamiko ya Muungano.
Sasa
kazi ya Bunge ni moja tu nayo ni kuboresha rasimu iliyopo mbeleyake ili
kumaliza kero za muungano zilizopo na kujibu hoja za hofu za muundo
mpya. Hakuna sababu ya kubishana kwenye takwimu za Tume, tume imefanya
wajibu wake na sasa Bunge Maalumu nalo litimize wajibu wake.
Iwapo
kama kweli tunataka kusikia Watanzania wanataka nini kwenye muundo wa
Muungano, tusimamishe Bunge na twende tukawaulize kwa kura (referendum).
Vingivenyo tuboreshe rasimu iliyopo na iliyotokana na maoni ya wananchi
wote kwa kujibu hizo hofu muhimu alizoainisha ndugu Rais na hayo
malalamiko muhimu yaliyoainishwa na Tume. Sio kazi ya Bunge Maalumu
kutafuta ubora wa hotuba zilizotolewa mbele yetu bali kuona mazuri ndani
ya hotuba hizo yasaidie kazi yetu Tuzingatie kuwa tusijenge Nchi kwa
kujibu malalamiko na hofu tu maana hofu na malalamiko hayaishi katika
dunia inayobadilika kwa kasi sana.
Tuamue
tunataka kuwa Jamhuri ya Muungano ya namna gani. Nini sababu ya Jamhuri
yetu na aina gani ya Tanzania tunataka kujenga. Tuanze kwa kutafsiri
sababu ya Tanzania kuwepo na Tanzania gani tunataka kujenga kisha
tutunge Katiba itakayowezesha kutufikisha huko tutakapo kufika.
Post a Comment