Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipima damu mara
baada ya kufungua kampeni ya kutoa huduma za shinikizo la Damu na
Kisukari katika majengo ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Mnazi
Mmoja Mjini Zanzibar. Mradi
huo unasimamiwa na Jumuiya ya Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania
(TAMSA) kwa kushirikiana na Chuo mcha Kimataifa cha Udaktari Tanzania
(imtu)
Baadhi
ya Wanachama wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania (TAMSA) kwa
kushirikiana na wizara ya afya Zanzibar wakiendesha zoezi la siku nne la
kupima, kutoa elimu na huduma za Dawa kwa wagonjwa wa maradhi ya
Kisukari na Shinikizo la Damu hapa Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif akisalimiana na Mkuu wa Chuo
cha Kimataifa cha Udaktari Tanzania (IMTU) Profesa Flora Fabian Mbatia
kwenye majengo ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Mnazi Mmoja
Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ .
*******************************
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ukosefu
wa mlo kamili uliokusanya matunda na mboga za kutosha, uvutaji wa
sigara na unywaji wa pombe kiholela, tabia ya uvivu na ongezeko la uzito
ndio sababu kuu zinapelekea ongezeko kubwa la maradhi ya Kisukari na
shindikizo la Damu miongoni mwa wanaadamu.
Alisema
utumiaji wa vyakula hivyo kwa mpango maalum pamoja na ushauri
unaotolewa na wataalamu wa afya ndio njia pekee inayoweza kuzuia
kuripuka kwa maradhi hayo kwa zaidi ya asilimia 80%.
Balozi
Seif alisema hayo katika sherehe ya ufunguzi wa Kampeni ya kutoa huduma
za Shindikizo la Damu na Kisukari zilizoandaliwa na Jumuiya ya Chuo cha
Udaktari Tanzania na kufanyika ndani ya Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar Kampasi ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Vuga
Mjini Zanzibar.
Balozi
Seif Ali Iddi alilazimika kuzifungua sherehe hizo ndani ya Ukumbi
kufuatia amri ya Jeshi la Polisi Tanzania kuzuia mikusanyiko ya aina
yoyote kwenye maeneo mbali mbali Nchini katika kipindi hichi.
Awali
sherehe hizo zilipangwa kufanyika katika uwanja wa michezo wa Maisara
Suleiman Mjini Zanzibar ambapo Jeshi la Polisi likaamuru zivunjwe kwa
kuondosha mkusanyiko wa watu.
Balozi
Seif alisema maradhi ya Kisukari na Shindikizo la Damu ambayo yamekuwa
tishio la vifo vingi hapa Nchini yamesababisha matatizo mengi ya
Kiuchumi na Kijamii kiasi cha kuzibebesha mzigo familia, Taifa na Dunia
kutokana na gharama za matibabu yake.
Alieleza
kwamba Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni { WHO } za mwaka 2012
zinaonyesha zaidi ya watu Milioni 4.8 wamepoteza maisha kutokana na
maradhi hayo wakati ambapo Dola za Kimarekani zaidi ya Bilioni 471
zimetumika katika kupambana na janga hilo.
Alifahamisha
kwamba utafiti uliofanywa kwa upande wa Zanzibar imeonyesha kuwa
asilimia 33% ya Wananchi wa Zanzibar wanasumbuliwa na tatizo la
shinikizo la Damu na asilimia 3.7% wamepatwa na maradhi ya Kisukari.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba inakadiriwa ifikapo mwaka
2030 zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 500 zinatarajiwa kutumika
katika kupambana na na maradhi ya Kisukari na Shinikizo la Damu
ulimwenguni kote.
Alitanabaisha
kwamba hicho ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho jamii ikiweza
kujiepusha na vishawishi vya maradhi hayo Mtaifa yanaweza kuokoa kiasi
hicho ambacho kinaweza kutumiwa katika Nyanja mbali mbali za maendeleo.
Balozi
Seif alieleza kuwa huo ni mtihani mkubwa ambao Binaadamu wanahitajika
kuwa makini kwa kila aina ya ushauri unaotolewa na wataalamu tofauti wa
sekta za afya na kuhakikisha kwamba unafuatwa vilivyo.
Aliupongeza
Uongozi na wanachama wote wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania {
TAMSA } pamoja na Chuo Cha Udaktari Tanzania { IMTU } kwa moyo wao wa
kujali ustawi wa Wananchi Bara na Zanzibar na kuahidi kwamba Serikali
itajitahidi kuunga mkono juhudi zao hizo.
Alisema
Chama cha Wanafunzi wa Udaktari kimekuwa kikifanya kazi kubwa katika
kuzisaidia Serikali zote mbili kwenye sekta muhimu ya afya. Hivyo
Serikali haina budi kuiunga mkono katika kusaidia changamoto
zinazoikabili Taasisi hiyo hususan suala zima la kupatikana kwa Jengo
kwa ajili ya Ofisi yao.
Balozi
Seif aliuomba Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA }
katika Kitivo cha Utabibu kufanya mazungumzo na Taasisi hiyo ya Tamsa
ili kuangalia utaratibu wa kujiunga kwa lengo la kutoa nafasi ya pekee
ya Vijana wa Zanzibar nao kuihudumia Jamii inayowazunguuka.
Katika
kuunga mkono jitihada za Wanachama hao wa Chama cha Wanafunzi wa
Udaktari Tanzania { TAMSA } za kupima kutoa huduma na dawa bure za
Maradhi ya Kisukari na Shinikizo la Damu ndani ya siku Nne hapa Zanzibar
Balozi Seif aliahidi kutoa mchango wa shilingi Milioni 1,000,000/-
kusaidia Chama hicho.
Mapema
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania {
TAMSA } ambae pia ni msimamizi Mkuu wa Mradi wa Kampeni ya kutoa huduma
za shinikizo la Damu na Kisukari Nd. Siraji Mohammed Mtulia alisema
chimbuko la mradi huo linatokana na ongezeko kubwa la maradhi hayo
katika jamii Nchini.
Siraj
Mohammed alisema mradi huo unakududiwa kutoa huduma za afya, elimu
pamoja na Dawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na Maradhi ya Shinikizo la
Damu na Kisukari katika mikoa yote Mitano wa Zanzibar.
Alisema
licha ya mradi huo kupata ufadhili wa Taasisi za Kitaifa na Kimataifa
zinazojihusisha na masuala ya Afya lakini utaendelea kuwa wa kudumu kwa
kusaidia jamii kutoa elimu ya afya kwa njia ya kujitolea.
Akitoa
salamu katika sherehe hizo Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha Udaktari
Tanzania { IMTU } Profesa Flora Fabia Mbatia alisema mradi huo ni wa
kwanza kufanyika Nchini Tanzania ukilenga kuongeza ufahamu wa Taaluma
ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.
Profesa
Flora alibainisha kwamba mradi huo uko sambamba na dhana ya Serikali
zote mbili katika kushajiisha jamii kupitia sekta ya afya kupiga vita
maradhi mbali mbali yanayowasumbuwa Wananchi.
Naye
kwa upande wa Wizara ya Afya Zanzibar Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr.
Saleh Mohammed Jidawi aliitanabahisha jamii kushirikiana na Serikali
katika kupiga vita maradhi hayo ya Kisukari na Shinikizo la Damu
kutokana na hatai yake kushinda haya yale maradhi ya kuambukiza.
Dr.
Jidawi alieleza kwamba maradhi hayo yanaua, yanaleta ulemavu, gharama
za tiba yake iko juu sana kiasi kwamba jamii inapaswa kubadilisha tabia
kwa matumizi ya vyakula visivyo na tija.
Post a Comment