STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24 Aprili , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema wakati umefika kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanza kufikiria
uwezekano wa kuanzisha chuo cha Uvuvi Zanzibar.
Dk.
Shein amesema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa
Wizara hiyo katika mkutano wa kujadili Mpangokazi na bajeti ya mwaka
2013/14 ya Wizara hiyo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Julai
2013 hadi Machi 2014 uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Amesema
mazingira ya kisiwa cha Zanzibar, mahitaji ya ajira kwa vijana na azma
ya serikali ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa samaki,
vinalazimisha kuweko kwa chuo maalum cha uvuvi kitakachosaidia kutoa
mafunzo kwa wananchi wa Zanzibar wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na
hasa vijana.
Vile
vile Rais wa Zanzibar amesisitiza haja ya viongozi na wafanyakazi wa
taasisi za umma kuandika taarifa za ziara za kimafunzo wanazohudhuria
ndani na nje ya nchi na kuzifanyia kazi taarifa hizo ili ziweze
kuwajengea uwezo wafanyakazi wengine ambao hawakupata fursa hizo.
“tija
ya ziara zinazofanywa na watumishi wa umma katika sehemu mbali mbali
ndani na nje ya nchi inaweza kupatikana iwapo tu wanaofanya ziara hizo
wataandika taarifa kuhusiana na wanayojifunza kutokana na ziara hizo na
kuwataarifu wengine wasiopata fursa hizo’ alisema Dk. Shein.
Akizungumzia
umuhimu wa kuwa na mipango mizuri ya serikali, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameitaka Wizara hiyo kuhakikisha kuwa
inakuwa na mipango mizuri itakayoweza kutekelezeka kwa ufanisi.
Amesema mipango mizuri ya serikali ni ile itakayopangwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya watendaji wote kwenye taasisi husika.
Aidha,
amesema ni vyema taasisi zote za umma zikazingatia thamani halisi ya
bei ya bidhaa na huduma zitakazohitajika wakati wa kupanga na kutekeleza
majukumu ya taasisi zao ili kuwa na bajeti halisi kwa mahitaji halisi.
Akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji ya Wizara yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi Dk. Kassim Gharib Juma amesema Wizara yake imekuwa ikipata
mafanikio makubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi katika kipindi cha
mwaka 2013/14.
Aliyataja
mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa
kutoka tani 24,343 mwaka 2012 hadi tani 27,244 mwaka 2013 ikiwa ni
ongezeko la asilimia kumi na moja, uzalishaji wa mayai umeongezeka
kutoka tani 105, 125 mwaka 2012 hadi kufikia tani 130,464 mwaka 2013
ambalo ni ongezeko la asilimia 19 huku nyama ya ng’ombe katika kipindi
hicho imeongeeka kwa asilimia 17.
Katika
taarifa yake hiyo Dk. Gharib alieleza pia kuwa mafanikio makubwa
yamepatikana katika udhibiti wa maradhi yasiyo na mipaka pamoja na
maradhi ya kichaa cha mbwa kutokana na kuimarika kwa huduma za chanjo.
Kwa
upande wa sekta ya uvuvi, Dk. Kassim amesema kumekuwa na ongezeko la
uvuvi wa baharini na pia wananchi wengi wameshajiika kuendeleza ufugaji
wa samaki na mazao ya baharini.
Alibainisha
kuwa jumla ya tani 23,000 za samaki zilivuliwa kwa kipindi cha miezi
tisa kwa mwaka wa fedha 2013 – 2014 ambazo zimewaingizia wavuvi jumla
ya shilingi bilioni 89.7.
Post a Comment