HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
Watalii
Mabilionea 42 kutoka Marekani wamemaliza ziara yao ya utalii ya siku
nne katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuelezea kufurahishwa kwao
na uzuri wa hifadhi pamoja na maajabu ya wanyama mbalimbali
wanaopatikana Serengeti ikiwemo msafara maarufu wa wanyama wahamao aina
ya nyumbu.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu alipata fursa ya kuwaaga watalii
hao walipokuwa wakiondoka nchini kuendelea na ziara ya utalii katika
nchi nyingine za Afrika wakitumia ndege binafsi aina ya Boeing BBJ 737
HB-11Q inayomilikiwa na Kampuni ya Utalii ya Abercrombie & Kent ya
nchini Marekani.
Watalii
hao walioingia nchini Machi 28, mwaka huu wakiongozwa na Mwanzilishi na
Mwenyekiti wa Kampuni ya Abercombie & Kent, Geoffrey Kent
wameelekea katika nchi za Italia, Botswana, Malawi, Zambia, Uganda,
Namibia, Ethiopia na Afrika Kusini ikiwa ni muendelezo wa ziara yao ya
kitalii katika nchi za Afrika.
Hili
ni kundi la pili likifuatia ziara iliyofanywa na kundi jingine la
mabilionea waliotembelea Serengeti mapema mwezi wa tatu mwaka huu kwa
siku tatu na makundi yote yalifuatana na wanahabari kutoka kituo cha
Televisheni cha Marekani cha CNBC ambao wamekuwa wakichukua picha na
matukio mablimbali ya ziara hiyo kwa ajili ya kurusha katika kituo hicho
kupitia kipindi chao maarufu kinachofahamika kama “Secret Lives of the
Super Rich.”
Kipindi hiki hurushwa kupitia kituo hiki katika mataifa ya Marekani, Asia, Ulaya, Mashariki ya Mbali na Afrika.
Kwa
upande wake Waziri Nyalandu alisema ujio wa watalii hao matajiri ni
faraja kwa sekta ya utalii kwa kuwa itajenga imani kwa wenzao ambao
hawajafika nchini kutembelea vivutio vya utalii.
Hivi
sasa sekta ya utalii inachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na Marekani
ndiyo nchi inayoongoza kwa kuleta watalii wengi nchini wanaofika
kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini. Waziri
Nyalandu alibainisha kuwa malengo ya wizara yake ni kuhakikisha sekta
hiyo inachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa.
Nyalandu
alisema Serikali inakusudia kuhamasisha utalii wa makundi kwa kutumia
ndege binafsi na mabasi kulingana na uwezo wa watalii wenyewe.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
02.04.2014
Post a Comment