Dodoma. Mbunge
wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed amesema anapanga kujitosa kwenye
kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu hivi karibuni mjini Dodoma, Hamad Rashid
alisema: “Kama Mwenyezi Mungu akinijalia uhai na uzima mwakani,
ninatarajia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais ama wa Muungano au
wa Zanzibar.
“Ila sijaamua kama ni Bara au Zanzibar; kama ni chama cha CUF au kingine, hayo yote yatakuja baadaye,” alisema Hamad Rashid.
Mohamed
ambaye ana mgogoro mahakamani na chama chake cha CUF, ametoa kauli hiyo
wakati tayari viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), CUF
kikiwamo wanajipanga kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi
ujao.
Mbali na
CUF, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni NCCR-Mageuzi na Chadema ambavyo
pia vinakusudia kusimamisha mgombea mmoja kwa nafasi za ubunge na
udiwani, lengo likiwa kukabiliana na nguvu ya chama tawala, CCM.
Hamad
Rashid aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu CUF, alifutwa uanachama Januari 4,
2012 na Baraza la Uongozi la chama hicho kwa madai ya kukihujumu kwa
mujibu wa kifungu 63 (1) (j) na 64 (1-5) cha Katiba ya CUF. Wengine
waliotimuliwa pamoja na Hamad ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Hamis Juma na
Juma Said Sanani.
Sakata la
Hamad kuvuliwa uanachama lilianza baada ya kutangaza kuwania nafasi ya
Katibu Mkuu wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu, nafasi
inayoshikiliwa na Seif Shariff Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais, Zanzibar.
Hata
hivyo, Januari 10, 2012 Hamad Rashid na wenzake waliiomba Mahakama
iwatie hatiani wadhamini wa CUF, kwa kukiuka amri ya Mahakama kutokana
na uamuzi wa Baraza la Taifa la Uongozi la chama hicho kuwafukuza
uanachama wakiwa tayari wameweka zuio.
Baadaye
Septemba mwaka jana, Hamad alikaririwa na gazeti moja akisema suluhu
yake na CUF haiwezi kupatikana kwa kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo
hakubaliani nayo ndani ya chama hicho.(MWANANCHI) (FS)
Post a Comment