Mbunge wa
Mwibara (CCM), Kangi Lugola amesema iwapo Muswada wa Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT), hautapelekwa bungeni, atakusanya saini za wabunge ili
kumwondoa madarakani Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Lugola
aliyasema hayo jana alipokuwa akiomba mwongozo wa Spika ni lini muswada
huo unaolenga kufuta misamaha ya kodi utaletwa bungeni.
Alisema amepata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ya
Mitaa
(Laac), Rajab Mborouk Mohamed ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi kuwa
kamati hiyo iliiagiza Serikali kuwasilisha haraka Muswada wa VAT.
Alisema lengo la kutaka muswada huo uletwe bungeni ni kupitia na kufuta misamaha yote ya kodi isiyo na tija.
Alisema
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka
2012/2013 inaonyesha kuwa kuna misamaha ya kodi ya Sh1.5 trilioni
nchini.
"Bajeti
yetu ya mwaka jana inaonekana ina upungufu wa Sh1.5 trilioni na
kusingekuwa na misamaha ya kodi mwaka jana tusingekuwa na upungufu huo,"
alisema.(Martha Magessa)
"Wabunge
tumekuwa tukiilazimisha Serikali iongeze fedha. Wabunge ndiyo
waliomchagua Spika na Spika ameonyesha kuipendelea Serikali ilhali
wananchi wanashindwa kupata maendeleo," alisema.
Alihoji ni lini muswada huo utaletwa bungeni kwa sababu karibu Bunge la Bajeti linaelekea ukingoni.
"Haya
mambo ya wabunge kutishwatishwa kwamba tukikataa Bajeti ya Serikali
Bunge litavunjwa. Mimi niko tayari Bunge livunjwe nirudi Mwibara
nikalime na kuvua dagaa," alisema.
Alisema
kama muswada huo hautaletwa katika Bunge la Bajeti atakuwa mbunge wa
kwanza kuleta hoja ya kumtaka spika afukuzwe kwenye kiti hicho kwa
sababu anaibeba Serikali.
Alipoulizwa
baadaye jana jioni sababu ya kumng'ang'ania Spika, Lugola alisema:
"Ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ambayo hupanga ratiba. Ukitazama
ratiba ya mkutano huu, hakuna mahali panapoonyesha Serikali italeta
muswada huo wa VAT badala yake, Serikali inasema tu kwa mdomo na yeye
ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi," alisema Lugola.
Akijibu,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi alisema Serikali ndiyo iliyoomba kuleta Muswada wa VAT katika
Bunge hili bajeti... "Hana sababu ya kumsingizia Spika kuibeba Serikali.
CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment