Dodoma.
Mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CUF, Amina Abdallah Amour amemjia
juu katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa kuufananisha
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kundi la Boko Haramu na kutaka
alaaniwe.
Ukawa
iliundwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba na unahusisha wajumbe kutoka
vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.(Martha Mageesa)
Akizungumza bungeni mjini Dodoma juzi, mbunge huyo alisema kauli ya Nnauye ni ya uchochezi na inapaswa kulaaniwa.
Mbunge
huyo alikuwa akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto kwa mwaka 2014/2015 iliyowasilishwa
na waziri wake, Sophia Simba.
"Gazeti
la Uhuru (jana) lilimnukuu Nape Nnauye akisema Ukawa ni sawa na Boko
Haramu... Hii ni kauli chafu na ya uchochezi. Haikubaliki na ninailaani
kwa nguvu zangu zote," alisema.
Mbunge
huyo alihoji "wazazi wao hawajui watoto wao wanaishije, wanakula nini
wala wanalala vipi.... Leo hii Nape Nnauye amethubutu kusema Ukawa ni
sawa na Boko Haramu?"
Hata hivyo, wakati akihoji hivyo, baadhi ya Wabunge wa CCM nao walisikika wakihoji "na Intarahamwe Je?".
Ukawa
ilitumia jina hilo la Interahamwe wakati mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba akitangaza uamuzi wa kundi hilo kujitoa kwenye Bunge la
Katiba, akiifananisha CCM na kundi hilo la nchini Rwanda.
Katika
gazeti hilo, Nnauye amenukuliwa akisema Ukawa ni kundi hatari
linaloeneza chuki na kusambaza uongo kwa Wananchi kwa nia ya kuwagawa na
kusema silaha wanazotumia ni zaidi ya Boko Haramu.
Nnauye
anadaiwa kutoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani
Tabora, akisema silaha za uongo wanazotumia viongozi wa Ukawa ni hatari
zaidi kuliko silaha za moto zinazotumiwa na Boko Haramu.
Viongozi
wa CCM na wale wa Ukawa wamekuwa wakizunguka nchi nzima kufanya mikutano
ya hadhara kufafanua kile kilichojitokeza ndani ya Bunge la Katiba na
kusababisha Ukawa kususia Bunge hilo.
CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment