Watu wengi wangetamani kuona hawazeeki, wanabakia na nguvu za ujana na kwa sababu hiyo wanasayansi wanatafiti kupata ufumbuzi.Vyuo
vikuu vitatu maarufu duniani vimekuja na matokeo ya utafiti ambao
unaweza kukata kiu ya wengi ambao hawatamani kamwe kuzeeka. Siku hizi
kumekuwapo na usemi kuwa uzee mwisho Chalinze, jijini (Dar es Salaam)
kila mtu ‘baby’ (mtoto). Hii ikiashiria watu hawapendwi kuitwa wazee
ingawa umri wao ni mkubwa. Wamekuwa na kauli hiyo ili kulazimisha
mazingira kwamba bado wana uwezo wa kufanya yote kama wenye damu changa
lakini katika uhalisia si kweli.Utafiti
wa vyuo vya Harvard na California vya nchini Marekani vikishirikiana na
Cambridge nchini Uingereza, unajenga mazingira ya kuifanya ndoto ya
wenye mawazo ya kuukataa uzee kuwa kweli. Watafiti hao walichukua damu
ya panya mchanga na kumuingizia kwa aliyezeeka. Walichobaini ni kwamba
panya yule mzee alichangamka na kurejewa na nguvu za ujana.
Matokeo
ya utafiti huo yanatoa mwanya kwa wanasayansi kukaa kitako na
kutengeneza dawa ambayo mtu akitumia anaweza kutozeeka. Kutozeeka huko
ni kuendelea kuwa na dalili za ujana kama vile kutokuwa na makunyanzi
usoni na viungo kuendelea kuwa na nguvu ya kutekeleza mambo yote kama
kawaida hata wenye umri wa zaidi ya miaka 70.
Utafiti ulivyofanyika
Timu
ya watafiti hao wiki hii walitangaza kuwa wamegundua namna ambayo
wanaweza kumfanya panya mzee kutokuwa na dalili zinazofanana na umri
huo. Wanasema kwenye utafiti huo kuwa mara baada ya kuchukua damu ya
panya mchanga na kumuingizia aliyezeeka ghafla alibadilika na kurejewa
na nguvu zilizomfanya achangamke na kutenda kama vile bado hajazeeka.
Walichobaini
ni kwamba ile damu ilienda kuchangamsha ubongo kiutendaji na kuwezesha
kuimarika kwa utendaji wa mwili kwa jumla.Kwa kawaida mambo yote
yanayotendeka mwilini huongozwa na ubongo kwa kuhamasisha homoni fulani
kulingana na jambo husika.
Wanasema
kwenye damu ya panya mdogo kuna aina ya protini ijulikanayo kama GDF11,
ambayo wanahisi ndiyo iliyochochea jambo hilo. Wakasema wanachofanya ni
kuchunguza kama hii protini ndiyo inayochochea ujana.
Mtaalamu wa Tanzania
Akizungumzia
juu ya utafiti huo, mtaalamu wa Afya ya Jamii katika Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii Dk Alex Mwita anasema hakuna haja ya watu kujipa
matumaini kutokana na ugunduzi huo kwa sababu hadi kupatikana dawa
itakayotumika kwa binadamu inaweza kuchukua miaka zaidi ya 10.
“Huu
ni ugunduzi kwa panya. Hadi kufikia mafanikio kwa binadamu, ni utafiti
utakaochukua miaka mingi,” anaonya Dk Mwita. Alisema zipo tafiti nyingi
kuhusukile kinachosababisha uzee na kujaribu kutafuta njia za kuuzuia
lakini bado mafanikio hayajapatikana.
Nini kinasababisha uzee
Wataalamu
wanasema kuwa ni jambo ambalo liko wazi kwamba uzee unapozidi, mwili
hushindwa kujimudu na hatimaye kusababisha kifo. Utafiti uliosimamiwa na
mtaalamu wa Elimu ya Viumbe katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini
Marekani, Dk John Langmore ulibaini kuwa mtu anakufa kwa umri kutokana
na viungo vya mwili kushindwa kutekeleza kazi zake kikamilifu.
Hali
hiyo inachangiwa na kasi ya seli za mwili kuzaliana kupungua kwa
kiwango kilichopindukia huku zinazokufa zikiwa nyingi. Mfumo huo uko
hivi, mtoto anapozaliwa ukuaji wake ni wa kasi sana. Hii inatokana na
uwiano wa seli zinazokufa kuwa kidogo zaidi ukilinganisha na zile
zinazozalishwa. Uwiano wa seli zinazokufa na zinazozalishwa hufikia
mahali ukalingana. Ikifikia kiwango hicho mtu huwa hakui tena.
Uzee
unaanza pale uwiano wa seli zinazokufa kuwa wa juu zaidi kuliko zile
zinazozalishwa. Hali hiyo huanza kuusababisha mwili kusinyaa na
kusababisha mikunjo sehemu mbalimbali za mwili. Kasi ya seli zinazokufa
ukilinganisha na zinazozaliwa huendelea kuongezeka na hali hiyo
huendelea kuongeza makunyanzi na hata baadhi ya viungo kupoteza uwezo
wake wa kawaida.
Kinachosababisha seli kutozaliana
Dk
Langmore na timu yake wanaamini kufa kwa seli ni jambo la kawaida
lakini sababu ya kasi ya kuzaliana kupungua kulingana na umri, ni jambo
muhimu pia.Waliamini ufumbuzi huo ndiyo utakaowapa sababu ya mtu kuzeeka
na pingine kutafuta namna ya kuzuia uzee.
Walibaini kuwa DNA ndani ya seli ndiyo inayohusika katika kuwezesha seli kuzaliana au kutozaliana.
Wakabaini
kuwa ina kichocheo ambacho kinasababisha mazingira hayo ya seli
kutozaliana hasa mtu anapofikia umri mkubwa. Dk Mwita anasema kulingana
na tafiti mbalimbali zilizofanyika kuna kitu kinachojulikana kisayansi
kama Telomere.
Anasema
Telomere inauhusiana na seli kudumu muda mrefu ikiwa na uwezo wa
kuzaliana au la. “Telomere ni kama kamba ya kufunga viatu. Inapomalizika
unakua mwisho wa seli kuendelea kuzaliana,” anasema Dk Mwita.
Anafafanua kuwa watu wanaokuwa na Telomere ndefu ndiyo wanaishi muda
mrefu na wale wanaokuwa na fupi, maisha nayo yanapungua.
Mtafiti
mwingine wa Marekani, Dk Ronald Klatz anaonya wanasayansi kutojikita tu
katika kuchunguza sababu za uzee kwa kutumia jeni na mfumo wa seli za
mwili. Akasema ipo haja pia kuchunguza mienendo ya mwili unavyoguswa na
namna za ulaji, mazingira na misongo ya mawazo. Akasema hali hizo kwa
namna moja au nyingine zinachangia mwili kuchoka na hata kupunguza
kiwango cha kawaida cha mtu kuishi.
Imeandikwa kwa msaada wa mitandao
MWANANCHI
Post a Comment