MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amewataka
wakulima, wafugaji kuipiga mawe Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kwa kutenga sh bilioni 50 kwa ajili ya safari za rais huku ikitenga sh
bilioni 51 kwa maendeleo ya kilimo.
Akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015,
Mdee alisema serikali haina nia ya dhati ya kuutokomeza umasikini,
ikiwemo kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi.
Alibainisha kuwa katika bajeti ya mwaka jana, serikali iliahidi
asilimia 10 ya bajeti itakwenda kwenye kilimo, lakini ikaishia kutenga
asilimia nne, na bajeti ya mwaka 2014/2015 imetenga sh bilioni 51 kwa
ajili ya miradi ya maendeleo ya kilimo.
Alisema kiwango hicho kimepishana kidogo na kile kilichotengwa kwa
ajili ya safari za Rais Jakaya Kikwete, ambazo zimetengewa sh bilioni
50.
“Wakulima, wafugaji na wavuvi wanapaswa kuipiga mawe Serikali ya CCM,
hapa mmetuletea bajeti, lakini ukiangalia kwa kina utaiona haina
dhamira ya kuwasaidia wananchi,” alisema.
Mdee, alisema bajeti ya Wizara ya Kilimo kila mara imekuwa ikitengewa
fedha, lakini hazifiki kwa walengwa, hivyo mipango mbalimbali
imeshindwa kutekelezeka.
Alisema kuwa serikali kupeleka huduma kwa wananchi ni lazima na sio
hiyari, hivyo wabunge wa upinzani wanapokosoa utendaji wa serikali
hawafanyi jambo baya bali wanatekeleza wajibu wao.
Aliongeza kuwa serikali kila mara imekuwa ikipewa ushauri mbalimbali,
lakini inashindwa kutekeleza jambo linalosababisha kukosa mapato
yanayotakiwa.
Alisema miaka minne iliyopita upinzani ulipendekeza kodi ya mishahara
kwa wafanyakazi ishuke chini ya asilimia 10, lakini serikali ilishindwa
kutekeleza jambo hilo hadi hivi sasa ilipoamua kushusha kutoka asilimia
13 hadi 12.
Aliongeza kuwa Kamati ya Bajeti inafanya kazi kwa niaba ya Bunge na
imelalamika inatoa mapendekezo serikalini lakini inapuuzwa hali
inayoonyesha serikali haina dhamira ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato
visivyowaumiza wananchi.
Mkosamali amvaa Chenge
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliituhumu Kamati
ya Bajeti kuwa inafanya vikao visivyo na tija ilimradi ihalalishe
wajumbe wake kupewa sh 500,000 kwa kila kikao.
Alisema anashangazwa na kamati hiyo kuendelea kulalamikia kupuuzwa
kwa ushauri wanaoutoa kwa serikali wakati wana uwezo wa kutoa azimio la
kukataa bajeti hadi walichokishauri kifanyiwe kazi.
“Jamani tuwe wakweli hapa, sisi tunalalamika tu wakati uwezo wa
kubadilisha mambo tunao, tukubaliane hapa kuikataa bajeti hii mpaka
serikali itakapoleta bajeti yenye tija kwa taifa.
“Kamati ya mzee Chenge taarifa yao inalalamika kuanzia mwanzo mpaka
mwisho halafu inasema inaunga mkono bajeti, hivi kama si unafiki ni
nini? Inakaa hivi sasa na mashirika kujadili kuwapunguzia kodi… hii ni
rushwa tupu,” alisema.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema serikali
imeshindwa kutumia ushauri wa kuanzisha kituo cha uvuvi wa samaki katika
bahari kuu, ambako samaki wanavuliwa bila kulipiwa ushuru na kampuni
kubwa.
“Nyinyi serikali mna tatizo gani kila mwaka tunawapa ushauri na
wataalamu wenu wanaandika ripoti zinazoonyesha umuhimu wa kuanzia kituo
cha uvuvi katika bahari kuu, huko tunapoteza mapato mengi lakini
hamjali, nyinyi akili zenu zinawaza nini?” alihoji.
Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM), alisema kiwango cha
asilimia kilichopunguzwa kutoka katika kodi inayotozwa kwenye mishahara
ni kidogo na hakina msaada kwa wafanyakazi.
Alisema serikali inapaswa kujikita zaidi kwenye kutafuta vyanzo vipya
vya mapato badala ya kila kukicha kuwabana wafanyakazi na wananchi.
1 comments:
Waswahili wana methali kuwa kukaa bure si sawa na kutembea bure. Rais kama kiongozi wa nchi anapokwenda nje haendi kutalii ila kujenga mahusiano kutafuta pale tulipopungukiwa ili kuimarisha uchumi wetu. Hoja zinazotolewa zinaonyesha kama anaenda kutembea bila malengo! Hebu tuchukue tathimini kama akipewa kiasi hicho cha bil. 50 lakini mwisho wa siku akasababisha nchi ipate Bill 500 au Trillion kadhaa kosa ni lipi? Hicho kitawasaidia wakulima hao na sekta nyingine. Nafikiri uwezo wa kufikiri tunapishana! Tuchambue hoja kama wasomi na wachumi tunapokuwa bungeni sio kuwadanganya watu wasiojua umuhimu wa ziara za Rais nje ya nchi! Huyu ni sawa na mzazi au mume ndani ya nyumba akijifungia tu kutwa hatoki hata mke atajiuliza huyu mume kakaa ndani tu! je familia itaishi vipi? Ndipo waswahili wakasema Mgaa gaa na upwa hali wali mkavu! Tumeona mengi Rais wetu ametuletea wala mwenye kutambua hawezi kudanganyika na ghiliba za kisiasa zinazotolewa kwa kutafuta umaarufu na kuonyesha kuwa sisi tuna uchungu zaidi ya wengine!
ReplyPost a Comment