Monduli. Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa
Jimbo la Monduli, Edward Lowassa (pichani) ametangaza kuanza kwa hatua za
kuyarejesha kwenye Mamlaka za Serikali za Vijiji mashamba 21 ya
wawekezaji yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 10,000, ambayo
hayajaendelezwa.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lomooti,
Kata ya Lolkisale wilayani humo alipokwenda kutembelea boma la kisasa la
mfugaji Isaya Lembekure, Lowassa alisema haiwezekani wananchi wa
Monduli kukosa ardhi wakati, kuna ardhi yao iliyohodhiwa na wachache
bila kuendelezwa.
“Monduli tumechoka na uuzwaji wa ardhi. Kila
mahali ni matatizo ya uuzwaji wa ardhi. Sasa tunatangaza kuanza mchakato
wa kuyarejesha mashamba yote ya wawekezaji ambayo hayajaendelezwa.
Tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuyarejesha,” alisema
Lowassa.
Tamko hilo la Lowassa, lilipokewa kwa shangwe na
wananchi wa Wilaya ya Monduli na limekuja wakati migogoro ya ardhi baina
ya wawekezaji na wananchi na wakulima na wafugaji imeshamiri nchini.
Licha ya kutoa agizo hilo, Lowassa ameendelea
kukemea uuzajiwa wa ardhi wilayani humo, unaofanywa kinyume cha taratibu
na Serikali.
“Kuanzia sasa kiongozi wa kijiji atakayebainika
kuhusika kuuza ardhi kinyemela, ang’olewe kupitia mikutano ya vijiji,”
alisema Lowassa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Monduli, Twalib Mbasha alisema tayari halmashauri hiyo
imeanza maandalizi ya kuyarejesha mashamba hayo kwa kuwataka wahusika
wa mashamba hayo kujieleza kwa nini hawajayaendeleza hadi leo.
“Halmashauri inakusudia kuyafuta mashamba yote
yasiyoendelezwa na yaliyotelekezwa, hii ni kutokana na kushindwa kufuata
masharti ya ardhi kama ilivyoanishwa na sheria ya Ardhi namba 4,999
fungu la 44 na fungu la 48. Nimetoa siku 90 watu hawa wajieleze,”
alisema Mbasha.
Aliyataja mashamba yanayotarajiwa kurejeshwa
kwenye mamlaka za Serikali za Vijiji kuwa ni Meru Enterprises namba 10,
ACU LTD namba 2390, TANFORM LTD 47, TANFORM 44 na Melembuki Kitesho
Mollel namba 974 katika Kijiji cha Lolkisale.
Mashamba mengine ni The Monduli Parents Sec
School, Musa Mamuya namba 2278 lipo Makuyuni, David Pello 2275, Hillary
Gadi namba 2474, Khalifan Said Masoud 2276, Masoud Said Masoud 2277 yapo
Kijiji cha Mswakini Juu.
Alitaja pia yaliyopo katika kijiji hicho ni ya Lucas Petro Kambei namba 2597 na Rungwa game Safari Ltd namba 2765.
Alisema mashamba mengine ni Omary Daudi Mshana
1571, Saidi Rashid Lena namba 2549 yaliyopo Kijiji cha Naitolia, wakati
mashamba mengine ni ya T.R Msuya namba 3, Esimingori Estate Ranch namba
7/2, Saburi Estate Ltd namba 7, Musa Y. Mamuya yaliyopo Makuyuni.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment