Na Evance Ng'ingo
Mamia ya waombolezaji walijitokeza jana katika makaburi ya Kinondoni kumzika aliewahi kuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, George Mpondela amezikwa jana katika makaburi ya Kinondoni, Dar es salaam.
MArehemu Mpondela alifariki dunia ijumaa iliyopita katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es salaam alipokuwa amelazwa kwa siku kadhaa kutokana na ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua. Mpondela aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga mwaka 1994 na atakumbukwa kutokana na misimamo yake iliyosaidia kusukuma gurudumu la maendeleo la klabu hiyo kongwe nchini.
Akizungumza katika maziko hayo Mwenyekiti wa sasa wa Yanga, Yusuph Manji alisema kuwa Mpondela atakumbukwa kwa mawazo yake yaliyokuwa na mwelekeo chanya kwa maendeleo ya klabu hiyo. Alisema kuwa marehemu Mpondela alikuwa akihamasisha uanzishwaji wa Yanga kampuni kwa lengo la kuendeleza zaidi klabu hiyo.
"Mbali na kuwa alikuwa Katibu Mkuu muda mrefu uliopita lakini pia alikuja kuwa mmoja kati ya watu wenye mchango zaidi kwa maendeleo ya klabu hiyo hadi alipofariki.
"Huyu hakuwa mtu wa kushindwa kitu alikuwa akipenda kazi yake na alikuwa na mawazo ambayo ni ya kuendeleza klabu tu aliweza kuiweka klabu pamoja na wanachama wake pia"alisema Manji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wazee wa klabu ya Yanga, Ibrahim Akilimali alisema kuwa Mpondela aliwatambua na kuwasaidia wazee hao klabuni hapo hadi alipofariki.
Alisema kuwa alikuwa akisaidiana na wazee hao katika kusukuma gurudumu la maendeleo na kuongeza kuwa hakuwa na dharau kwa kila mwanachama.
Katika makaburi hayo pia walijitokeza watu mbalimbali kumuaga Mpondela akiwamo Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi.
Post a Comment