Na Mwandishi Wetu
RAIS
Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maonyesho ya
kimataifa ya utalii yanayojulikana kama Swahili Tuorism Expo
yanayotarajiwa kufanyika Dar es Salaam Oktoba mwaka huu.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Razaro Nyalandu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
Dar es Salaam alipozindua rasmi tovuti ya taarifa za maonyesho hayo
inayojulikana kama Swahili Tourism Expo (S!TE).
Maonyesho
hayo yatakayohusisha kampuni binafsi, taasisi za kiserikali kama Bodi
ya Utalii Tanzania (TTB) pamoja na washirika wengine katika sekta hiyo
yanatarajiwa kufanyika tarehe 1 mpaka 4 Oktoba, mwaka huu katika ukumbi
wa Mlimani City Dar es Salaam.
Waziri
Nyalandu alisema maonyesho hayo ni fursa ya kipekee kwa Tanzania
kupanua wigo wa sekta ya utalii ambapo nchi zote za ukanda wa Afrika
Mashariki pamoja na Sudan zinatarajiwa kushiriki lakini pia mataifa
mbalimbali yataalikwa.
Alisema
tayari 50% ya nafasi za maonyesho zimeshachukuliwa na kwamba mialiko
kwa mataifa mbalimbali imeshatumwa ambapo ofisi yake itafuatilia kwa
karibu mialiko hiyo na kuhakikisha nchi nyingi kwa kadri inavyowezekana
zinashiriki.
“Kutokana
na ukubwa wa tukio hili Rais Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
lakini pamoja na TTB kupewa jukumu la kuratibu pia ofisi yangu itachukua
jukumu la kipekee kufuatilia mialiko iliyotumwa nchi mbalimbali
kuhakikisha zinashiriki,” alisema Waziri.
Aliongeza
kuwa maonyesho hayo yanatarajiwa kuongeza biashara ya kitalii nchini
ambapo baada ya hapo Tanzania inatarajiwa kupokea watalii zaidi ya
milioni 2 kwani maonyesho hayo yataitangaza nchi husika kwa kiasi
kikubwa.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTB, Balozi Charles
Sanga alisema maonyesho hayo yatakuwa chachu ya kukuza utalii wa ndani
na kuwajengea tabia watanzania kutembelea vivutio tulivyonavyo.
Alisema
tumekuwa tukipokea watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja kujionea
utajiri wa maliasili tulizonazo lakini idadi ya watalii wazalendo
imekuwa ndogo sana ambapo pamoja na mambo mengine muamko na taarifa za
vivutio hivi zimekuwa haziwafikii na hivyo maonesho hayo yatakuwa chachu
ya kuongeza idadi ya watalii wa ndani.
“Maonyesho
kama haya ni maarufu katika nchi za wenzetu na yamekuwa yanawasaidia
sana katika kukuza sekta zao za utalii hivyo nasi tunaanza na litakuwa
linafanyika kila mwaka,”
“Kupitia
maonyesho haya sekta na biashara nyingi za kitalii zitapanuka lakini
kubwa zaidi tunaamini baada ya hapo watanzania wengi watakuwa na taarifa
za kutosha kuhusu maliasili tulizonazo na watahamasika na hatimaye
kuongeza idadi ya watalii wa ndani ya nchi,” alisema Balozi Sanga.
Wizara
ya Maliasili kupitia TTB imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha
sekta ya utalii inakuwa na mchango wa kipekee katika pato la taifa
ambapo pamoja na maonyesho hayo pia ina mikataba mbalimbali ya matangazo
na nchi mbalimbali duniani katika kuhakikisha taarifa za vivutio vyetu
zinawafikia watu wengi zaidi.
Post a Comment