Mahakama
ya Afrika Mashariki (EACJ), imeizuia Serikali ya Tanzania kujenga
barabara ya lami kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ikieleza kuwa
ujenzi huo utaathiri mazingira, maisha ya wanyamawwpori na baoanuai ya
hifadhi hiyo.
Katika
hukumu iliyotolewa jijini Arusha jana, jopo la majaji watatu wa mahakama
hiyo wakiongozwa na Jaji Kiongozi Jean Bosco Butasi, liliiamuru
Tanzania kutotekeleza mradi wowote wa ujenzi au ukarabati wa barabara
hiyo utakaokuwa na madhara kwa mazingira na baoanuai ya hifadhi ya
Serengeti.
"Zuio la
kudumu linatolewa dhidi ya mdaiwa (Tanzania) kutekeleza mipango ya awali
au pendekezo la ujenzi au ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami
kupitia Hifadhi ya Serengeti itakayosababisha madhara kimazingira na
baoanuai ya hifadhi hiyo," inasema sehemu ya hukumu hiyo.
Kila upande
umeamriwa kubeba gharama zake katika shauri hilo lililoshuhudia
mgawanyiko kati ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa yale
ya Tanzania kuunga mkono ujenzi huo kwa madai kuwa una faida kwa maisha
na jamii inayoishi maeneo itakayopita barabara hiyo
Kwa
mujibu wa mpango wa Serikali, barabara hiyo ingepitia Mto wa
Mbu-Engaruka-Loliondo- Kleins Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na
ile ya Tarime-Musoma-Mwanza, hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa
wananchi wa maeneo haya ambao baadhi hulazimika kupitia Nairobi nchini
Kenya.
Hukumu
hiyo ilitolewa baada ya Taasisi ya Africa Network For Animal Welfare
(ANAW), ya jijini Nairobi, Kenya kufungua kesi dhidi ya Serikali ya
Tanzania kupinga ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239,
ikidai itaathiri mazingira, uhai wa wanyama na baionuai wa Hifadhi ya
Serengeti kwa kuongeza shughuli za kibinadamu.
Akisoma
hukumu hiyo kwa niaba ya majaji wenzake, Jaji Isaac Lenaola alisema
Serikali ya Tanzania ina haki ya kutunga sera na kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya umma, lakini sharti izingatie
upembuzi yakinifu kuepuka athari za kimazingira na baoanuai.
Jaji wa
tatu katika jopo hilo ni Jaji John Mkwawa kutoka Tanzania ambaye
anakamilisha mkataba wake mwishoni mwa mwezi huu. Nafasi yake tayari
imejazwa na Jaji Fakih Jundu ambaye hadi uteuzi wake Aprili 30, mwaka
huu, alikuwa Jaji Kiongozi.
Hukumu
hiyo inasema kuwa licha ya haki ya nchi zote wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) kupanga na kutekeleza miradi na majukumu ya
msingi kwa maendeleo ya wananchi, mipango hiyo lazima izingatie hoja ya
kidunia ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, maendeleo endelevu, sheria
na sera za kimataifa kuhusu mazingira na maliasili.
Mahakama
imekubaliana na hoja za walalamikaji waliokuwa wakiwakilishwa kwenye
shauri hilo na wakili Saitabao Ole Kanchory kuwa ujenzi wa barabara hiyo
yenye urefu wa Kilomita 239, ungeathiri mazingira na baionuai ya
Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya kwa
kuwa kungeongeza shughuli za kibinadamu.
Hukumu
hiyo inasema kuwa licha ya ukweli kwamba Serikali ya Tanzania ilipanga
kuacha barabara yenye urefu wa Kilomita 53 inayopita ndani ya hifadhi
katika kiwango cha changarawe, bado magari mengi yangepita kwenye
barabara hiyo iwapo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa
barabara hiyo ungetekelezwa ungekiuka ibara za 5(3), 8(1), 111(2) na
114 (1) ya mkataba wa EAC, zinazozungumzia wajibu wa kila nchi
mwanachama kupanga na kutekeleza sera na miradi yote iliyo chini ya
mamlaka na wajibu wao kwa kuzingatia ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa
faida na masilahi ya jumuiya nzima.
Post a Comment