Katika
toleo Na. 1734 la gazeti la Jambo Leo la tarehe 10 Juni, 2014 katika
ukurasa wa tatu iliandikwa taarifa iliyokuwa na kichwa cha habari
“Utafiti wa gesi kuinufaisha Morogoro, Kilimanjaro”. Taarifa hiyo
ilieleza kuwa wakaazi wa mikoa tajwa watanufaika na ugunduzi wa mafuta
na gesi uliofanywa na Kampuni ya Swala katika maeneo hayo.
Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linapenda kuwafahamisha
wananchi kuwa taarifa ya kwamba Kampuni ya Swala imegundua gesi na
mafuta katika maeneo ya Morogoro na Kilimanjaro sio sahihi. Ugunduzi wa
mafuta hufanyika tu baada ya kuchimba kisima cha utafiti na hatimaye
mafuta au gesi iweze kutoka yenyewe kutoka ardhini.
Hatua
ya kuchimba kisima cha utafutaji hutokana na tafiti mbali mbali za
awali za mitetemo ya ardhi na kubaini kama maeneo hayo yana uwezekano
wa kuwa na mafuta au gesi ama la. Hata kama eneo linaonesha dalili
nzuri za awali ni lazima sehemu hiyo ichimbwe na matokeo
yake
ni kuwa na ugunduzi au la. Vilevile ugunduzi huo lazima uonyeshe kutoa
kiasi cha rasilimali ambacho kinaweza kuzalishwa kibiashara
(economically viable).
Kazi
zilizofanyika mpaka sasa na Kampuni ya Swala katika maeneo ya
Morogoro – Kilosa na Pangani - Kilimanjaro ni utafiti wa awali wa
kukusanya takwimu za mitetemo na kubaini kama maeneo hayo yana kina
(thickness) cha kutosha cha miamba tabaka ambayo utafiti wa mafuta na
gesi unaweza kufanyika. Hivyo utafiti wa kina unaendelea ili kubaini
kama kuna miamba mashapo (prospects) ya kutosha kwa ajili ya kuchimba
kisima cha utafiti. Uchimbaji wa kisima hicho unaweza kutoa mafuta
au/na gesi au maji matupu. Hatua ya uchimbaji visima bado haijaanza.Hivyo basi si sahihi kwa mtu yeyote kusema kuwa kuna ugunduzi uliofanyika.
Utaratibu
wa kutafuta mafuta nchini ni wa kugawana mapato kati ya Mwekezaji na
Serikali kupitia Mikataba ya Kugawana Mapato (Production Sharing
Agreement-PSA) kama mafuta au gesi ikigundulika. Kampuni isipogundua
rasilimali yeyote, Serikali haimrudishii Mwekezaji fedha zake
alizowekeza kwenye ufafiti huo, hivyo hasara hiyo ni kwa Mwekezaji
mwenyewe.
Shirika
lina taarifa kuwa Kampuni ya Swala inauza Hisa zake katika soko la
Hisa la Dar es Salaam ili Watanzania washiriki katika shughuli za
utafutaji wa mafuta na gesi. Suala hili ni jema na Kampuni ya Swala
inastahili kupongezwa kwa kuwawezesha Watanzania kushiriki kwenye sekta
hii ambayo imeshika kasi katika miaka mitatu iliyopita. Aidha, Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania linawashauri Wananchi wafanye maamuzi
mazuri na kuwatumia washauri wao kuhusu ununuzi wa hisa hizo kwa
kuzingatia mambo yaliyoelezwa hapo juu.
Ikumbukwe
kuwa Tanzania tumechimba visima vya utafiti wa mafuta vipatavyo 78 na
vyenye gesi ni asilimia 40% tu huko Mkuranga (Pwani), Songosongo
(Lindi), Ntorya na Mnazi Bay (Mtwara) na Bahari ya kina kirefu.
Taarifa
kuwa katika mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro kumefanyika ugunduzi wa
mafuta na gesi haina ukweli wowote. Kama rasilimali ya mafuta au gesi
asilia ikigundulika mwenye mamlaka ya kutangaza ugunduzi huo ni
Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini pekee.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na: -
Mkurugenzi Mtendaji,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,
BWM Tower A,
S.L.P 2774,
Dar es Salaam.
Barua pepe: tpdcmd@tpdc-tz.com
Post a Comment