Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi
MPANGO wa
kuligawa Shirika la Umeme (Tanesco) kuwa mashirika mawili umeiva, baada
ya Serikali kupitisha Mkakati na Mwelekeo wa Sekta Ndogo ya Umeme
(ESI).
Mpango
huo utekelezaji wake unaanza Agosti mwaka huu, na lengo lake ni
kuhakikisha uzalishaji wa umeme, unaongezeka kutoka megawati 1,583
zinazozalishwa kwa sasa hadi kufikia uzalishaji wa megawati 10,000
ifikapo mwaka 2025.
Ugawanyaji
wa Tanesco maandalizi yake yanaanza Julai mwaka huu na utekelezaji wake
utatimia Desemba 2017, ambako kutaanzishwa mashirika mawili.
Shirika
moja litakuwa linashughulikia uzalishaji wa umeme na lingine litakuwa la
kushughulika na usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Lengo
kubwa la kugawanywa kwa Tanesco ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa na
uhakika wa kupatikana kwa nishati ya umeme kwa bei rahisi, ikiwa ni
pamoja na kukuza pato la mtu mmoja mmoja.
Habari
zilizopatikana jana, zinasema mwishoni mwa wiki Baraza la Mawaziri
limebariki mkakati huo ;na sasa kilichobaki ni kwa Wizara ya Nishati na
Madini, kuutangazia umma juu ya kuwepo mpango huo, unaotekelezwa chini
ya mpango ujulikanao kama Electricity Supply Industriy (ESI).
Ili
kukamilisha mpango huo, Serikali kwa sasa iko kwenye maandalizi
kuhakikisha kuwa mpango huo kuligawanya shirika hilo unatekelezwa mwaka
2017, Tanesco haitakuwa na madeni yoyote.
Kwa
kuanzia mwaka huu, Wizara ya Nishati na Madini imetenga Sh bilioni
565,71 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, ikiwa ni pamoja na kulipa
madeni ya Tanesco ambayo Serikali inadaiwa.
Lengo la
mkakati huo, ambao unaihusisha Serikali, sekta binafsi, Tanesco, Ewura
na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ni kuinua pato halisi la Mtanzania
kutoka pato la dola za Marekani 640 la sasa hadi kufikia pato la dola za
Marekani 3,000 kwa mtu ifikapo mwaka huo.
“Tumekuwa
tunafanya vizuri kwenye sekta ya umeme, lakini tunaamini tukitekeleza
kikamilifu mkakati huu sekta ya umeme itachangia ukuaji wa pato la taifa
na pato la mtu mmoja mmoja,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini, Eliakim Maswi wakati akizungumza na gazeti hili jana.
Chini ya
mkakati huo, idadi ya watu waliounganishwa na umeme itaongezeka kutoka
asilimia 24 ya sasa hadi kufikia asilimia 50, huku idadi ya wananchi
wanaopata huduma ya umeme, pia itaongezeka kutoka asilimia 34 ya sasa
hadi kufikia asilimia 75 mwaka 2025.
Maswi
alisema mkakati huo utatekelezwa chini ya Sheria ya Umeme ya mwaka 2008
na Sera ya Nishati ya mwaka 2003, ambazo zinatoa fursa ya Serikali
kuvutia wawekezaji binafsi kushiriki katika kuzalisha umeme.
Lakini,
pia mkakati huo unalenga kupunguza Serikali kugharimia uzalishaji wa
umeme, badala yake sekta yenyewe ya umeme, ndiyo itakayokuwa inatoa
gawio kwa Serikali, kama ilivyo kwa nchi nyingine, kama vile Thailand.
Mkakati
huo pia unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme ; na
kuhakikisha kuwa mahitaji ya umeme nchini na kwenye viwanda, yanatimizwa
na wazalishaji wa sekta hiyo ya umeme.
Mkakati wa utekelezaji
Ili
kutekeleza mkakati huo, Serikali imegawa utekelezaji wake katika hatua
nne. Mkakati wa kwanza ni kuanzia Julai 2014 hadi Juni 2015, mkakati wa
pili Julai 2015 hadi Juni 2018, awamu ya tatu itaanza Julai 2018 hadi
Juni 2021 wakati awamu ya nne, ambayo ni ya mwisho utekelezaji wake
utaanza Julai 2021 hadi Juni 2025.
Katika
awamu ya kwanza, baadhi ya shughuli zitakazofanyika ni kuunda timu
maalumu ya wataalamu kutekeleza mpango huo, kupitia upya Sheria ya Umeme
ya mwaka 2008 na kutekeleza mfumo wa kupunguza mfumo wa hasara kutoka
asilimia 19 hadi asilimia 18.
Pia,
wataboresha mifumo itakayotumika kwenye gridi ya Taifa wakati Tanesco
itakapogawanywa. Pia, kutafanyika tathmini za masoko, uwezo wa
rasilimali watu na uanzishwaji wa mfumo wa masoko ya umeme.
Katika
awamu ya pili ni kupunguza mifumo ya hasara kutoka asilimia 18 hadi 16,
kuigawa Tanesco kuwa na mashirika mawili na kupunguza utendaji wa
Tanesco kutoka makao makuu na kuzipa ofisi za kanda mamlaka zaidi kabla
ya mganyiko kufanyika.
Kwenye
awamu ya tatu shirika la uzalishaji wa umeme, litafanya tathmini kwenye
ofisi zake za kanda, kuweka mfumo wa uuzaji wa umeme kwa bei ya rejareja
huku kampuni mbili zitakazokuwa zimeundwa, zitapewa jukumu la
kuhakikisha mifumo ya hasara inapungua kutoka asilimia 16 hadi 14.
Katika
awamu ya nne, Ewura itatakiwa iandae viwango vya uzalishaji wa umeme
katika sekta ndogo ya umeme, kupunguza mifumo ya hasara hadi asilimia 12
na kuhakikisha asilimia 50 ya watu wanakuwa wameunganishiwa umeme ;huku
watumiaji wa nishati hiyo wanafikia asilimia 75 kupitia shirika la
usambazaji pamoja na REA.
Kwa nini mpango huo?
Kuwepo kwa ya Sheria ya Umeme na Sera ya Nishati ambazo zinatoa fursa ya kuanzishwa kwa Sekta Ndogo ya Umeme (ESI).
Kuwepo
kwa mpango wa fedha ambao hadi kufikia mwaka 2017 mahitaji ya fedha
katika sekta ya umeme, itakuwa ni dola za Marekani bilioni 11.4, kiasi
ambacho ni sawa na dola za Marekani bilioni 1.9 kwa mwaka zinahitajika
kutekeleza mpango huo.
Nchi
kujiwekea malengo kuwa idadi ya watu watakaounganishwa ifikapo mwaka
2015 asilimia 30, asilimia 50 ifikapo mwaka 2025 huku itakapofika mwaka
2033 asilimia 75 ya Watanzania watakuwa wameunganishwa na umeme.
Kwa hali hiyo mkakati huo unafanya Tanesco igawanywe na kuwa mashirika mawili ili kukidhi mahitaji halisi ya nishati ya umeme.
(CHANZO: HABARILEO) (FS)
Post a Comment