*************
Serengeti:Ni jambo la kawaida kuwaona wanaume
wilayani Serengeti wakiongozana na wake ama watoto wao siku za minada,
kwenda kuuza mifugo ili wanunue mahitaji yao, lakini mapato hudhibitiwa
na wanaume.
Mara baada ya mauzo na kununua mahitaji,wanawake
na watoto hulazimika kurudi nyumbani huku wanaume wakibaki wakistarehe
,huzitumia siku ,ni nadra mwanaume kuwahi kurudi nyumbani .
Mei 19, Rhoda Nyangi Mtatiro (24) mkazi wa
Kitongoji cha Kenyana kijiji cha Masangura kata ya Ring’wani wilayani
Serengeti, licha ya ujauzito wa miezi sita alionao alikubali kuongozana
na mumewe Wang’enyi Sabai(30) kutoka kijijini kwao hadi Rung’abure
umbali wa kilometa zaidi ya 15 kwa mguu.
Huku wakiswaga kondoo wanne walifanikiwa kufika
mnadani na kuwauza wakajipatia fedha za mahitaji hakujua kuwa kuna
balaa lingemkuta siku hiyo, pamoja na kuswaga na kutembea umbali mrefu
na ujauzito wake hakuambulia kitu zaidi ya kipigo ambacho leo hajui
hatima ya maisha yake.
Licha ya kufanikiwa kuuza kondoo wote aliambulia
Sh 2,000 kwa ajili ya kununua nguo za mtoto wao mmoja kati ya wanne
walionao anayesoma darasa la kwanza shule ya Msingi Geitasamo, iliyoko
hapo Rung’abure ambako ni kwao na Rhoda.
Ilikuwaje?
“Nilizunguka kutafuta nguo za mtoto, wakati huo
mume wangu alikuwa nyumbani kwetu anamsalimia mama mkwe…. Saa 11:30
jioni nilifika nyumbani na kuwaambiwa ameishaondoka kurudi kijijini
kwetu….nilishindwa kuondoka pekee yangu kwa muda huo na hali niliyonayo
nikalala kwetu, ikawa mwanzo wa matatizo,”anasema.
Anasema alilazimika kutoka saa 12 alfajiri na
kufika kwake saa tano asubuhi akiwa amechoka ,na kwenda kumsalimia mume
wake dukani, hata hivyo alivyopokewa akahisi atapata adhabu kwa kuwa
mume wake hana namna nyingine ya kuwasilisha hisia zake zaidi ya
kutembeza kipigo, akaamua kuaga na kurejea nyumbani.
“Nilishangaa kuona mume wangu akifunga duka huku
akiwa ameshikilia panga na kamba ananifuata …mita kadhaa akanifikia na
kuniamru nisimame, eneo lenyewe limejaa vichaka….niliingiwa na hofu,
ghafla akauliza nilikolala…kwa kujiamini nikamwambia nililala nyumbani
kwetu baada ya kuogopa kutembea pekee yangu jioni,” anasema na kuongeza:
“Akasema ameambiwa nilikuwa na mwanaume
gesti….nilimtaka anielewe kuwa nililala kwetu baada ya kuniacha…na
ujauzito huo ninawezaje kwenda na mwanaume gesti….ikawa kama amechokozwa
maana aliniamuru ninyanyue mikono juu na kuanza kunishambulia kwa
mateke tumboni, kama vile haitoshi akaanza kunikata miguu kwa panga ili
niseme kuwa nilikuwa na mwanaume gesti,” anasema kwa masikitiko.
Afungwa kwenye kiti
Pamoja na maumivu ya kupigwa tumboni na kukatwa
miguu, alifungwa kwenye kiti na kuendelea kuadhibiwa mbele ya mama mkwe
wake Rhobi Sabai na mke Mwenzake Rhobi Kibina(20), hadi akapoteza
fahamu, hata hivyo alijikuta amefungiwa ndani ya nyumba na kuambiwa kuwa
aliokolewa na jilani yao Moya Marwa.
Post a Comment