*********
Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
imetangaza matumizi ya teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration
(BVR), katika maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapigakura ambayo
yatafuta matumizi ya vitambulisho vya kupigia kura vya sasa.
Kwa hatua hiyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian
Lubuva ametangaza kuwa: “Katika kura ya maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi
Mkuu wa 2015, mpigakura atatumia kitambulisho kipya atakachopatiwa na
Tume baada ya kuandikishwa upya katika mfumo huu na si vinginevyo.
Vitambulisho vilivyotolewa katika uandikishaji na uboreshaji uliopita havitatumika tena.”
Akitangaza mpango huo mpya Dar es Salaam jana,
Jaji Lubuva alisema Tume hiyo itaanza maboresho ya daftari hilo kwa watu
wote wenye sifa za kupiga kura Septemba mwaka huu na kukamilisha kabla
ya kura ya maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu 2015.
BVR ni mfumo wa kuchukua taarifa za mtu za kibaiolojia hasa alama za vidole.
Mwaka 2004, NEC ilianzisha Daftari la Kudumu la
Wapigakura ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa taarifa za wapigakura na
uhifadhi wa taarifa za kielektroniki.
Sanjari na hilo, tume hiyo ilitoa vitambulisho vya
wapigakura ambavyo pia vimekuwa vikitumika kwa shughuli mbalimbali za
utambulisho katika maeneo kama benki, polisi, mahakamani, uhamiaji,
ukataji leseni, usajili wa simu na mengineyo.
Jaji Lubuva alisema katika kazi hiyo ya
uandikishaji, NEC imekusudia kutumia Sh293 bilioni kwa ajili ya ununuzi
wa vifaa, mafunzo ya watendaji na uandikishaji.
Maofisa watakaotumika katika uandikishaji ni
pamoja na waratibu wa uandikishaji wa mkoa, maofisa waandikishaji ambao
watakuwa ni wakurugenzi wa halmashauri, maofisa wasaidizi watakaokuwa
watatu kwa kila jimbo, watendaji kata na waratibu wa elimu.
Mafunzo kwa watendaji hao yanatarajiwa kuanza Julai, 2014 na uandikishaji utaanza Septemba na katika vituo 40,015 kote nchini.
Vituo vya uandikishaji
Jaji Lubuva alisema kwa utaratibu wa sasa, vituo
vya kujiandikishia vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ambavyo
vimewekwa katika ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa ili kuwezesha kuwa
karibu zaidi na wananchi.
Post a Comment