Kikosi cha Nigeria katika kombe la dunia kimesusia kikao cha mazoezi kama ilivyopangwa kwa sababu ya kukosa kulipwa fedha zao za ziada.
Kitengo cha michezo cha BBC kimeelezwa kuwa wachezaji hao wanaamini kuwa wamelipwa kiasi cha dola 15,000 (pauni 8,800), chini ya pesa wanazopaswa kulipwa baada ya kufika katika mkondo wa pili wa kombe la dunia, huko Brazil.
Wachezaji hao wamesusia mazoezi katika uwanja wa Campinas na baadaye maafisa wakadai kwamba mazoezi hayo yalikuwa yametupiliwa mbali.
Nigeria inachuana na Ufaransa katika mechi ya muondowano siku ya Jumatatu baada ya kuchukua nafasi ya pili katika kundi lao la F.
Shirika la habari la BBC michezo limeelezwa kuwa shida imetokea katika ufafanuzi wa njia itakayotumika kuwalipa wachezaji hao pesa hizo za ziada.
Wachezaji
hao wanaamini kuwa watapokea dola 10,000 kwa ushindi wao wa 1-0 dhidi
ya Bosnia-Hercegovina na dola 5,000 kwa sare yao dhidi ya Iran.
Hata hivyo,
inaaminika kuwa ahadi hiyo ya shirikisho la soka la Nigeria kwa
wachezaji wake ilijumuisha malipo ya ushindi na kutoka sare na pia
asilimia 30 ya pesa watakazolipwa na Fifa kwa kufika katika raundi ya
muondowano.
Inaaminika kuwa kitita hicho kinatarajiwa kupanda hadi asilimia 40
kama fedha watakazolipwa na Fifa ikiwa Nigeria watashinda mchuano wao wa
raundi ya muondowano, aslimia 50 kwa ushindi wa robo fainali, asilimia
60 kwa ushindi katika nusu fainali na asilimia 70 kwa kushinda kombe
hilo la dunia.
Huku Wahusika wote wakifanya juhudi za kupata suluhu ya mtafaruko huo
, mkufunzi, Stephen Keshi anasisitiza kuwa swala hilo halitakuwa na
madhara yoyote katika timu hiyo.
BBC pia imethibitishiwa kuwa wachezaji hao watasafiri kwenda Brasilia
siku ya Ijumaa kama ilivyoratibiwa na kufanya mazoezi yao jioni
itakayofuata.
Si mara ya kwanza timu ya Super Eagles kuchukua msimamo kama huo
kuhusu fedha. Mwaka uliopita walichelewa kufika katika michuano ya kombe
la mashirika huko Brazil.
Post a Comment