WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yanaendelea japo kwa kiasi
kikubwa hatma yake inategemea kukamilika kwa mchakato wa Katiba mpya.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Juni 30, 2014) wakati akizungumza na
Mameya wa Majiji, Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya
Tanzania katika kikao cha siku moja kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Regal Naivera jijini Tanga.
Waziri
Mkuu yuko Tanga kwa ajili ya sherehe za Serikali za Mitaa ambayo kilele
chake kitafanyika kesho Julai mosi kwenye uwanja wa Tangamano jijini
hapa. Ameamua kukutana na viongozi hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya
kukutana nao aliyoitoa Mei 14, 2014 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
ALAT.
“Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa bado ni kitendawili kwa sababu kwa kiasi kikubwa
inategemea sana kukamilika kwa Mchakato wa Bunge la Katiba,” alisema na
kuongeza:
“Kama
Wizara tunaendelea na maandalizi tukiamini uchaguzi upo, kama hiyo
fursa isipotokea bado tutakuwa tumekamilisha maandalizi kwa upande
wetu.Tunaendelea kuandaa kanuni kwa kushirikisha wadau wote,” alisema.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la ukusanyaji mapato na
udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali. Kuhusu mapato, Waziri Mkuu
alisema katika mwaka wa fedha wa unaoisha sasa, hali ya ukusanyaji
mapato haikuwa nzuri.
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Mkuu alisema amewaandikia barua Wakuu wa Mikoa
akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu
juu ya makusanyo ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.
“Katika
taarifa hizi itabidi kila Halmashauri ieleze ilipanga kukusanya kiasi
gani, je imefikia lengo na kama sivyo ni kwa nini. Nia yetu ni kutrack
down makusanyo na kuona yamekwama wapi na yamekwamishwa na nini,”
alisema.
Kuhusu
udhibiti wa matumizi, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti hao
kuendelea kuwabana wahusika ili kudhibiti matumizi yasiyofaa. “Lazima
muendelee kuwabana na kuwasimamia wakurugenzi na wataalaam wa kwenye
Halmashauri zenu. Fanyeni kazi kwa ufanisi, msiwachekee wale
wanaoharibu,” aliongeza.
“Ili
muweze kuwabana vizuri, ni lazima mdai kupatiwa taarifa za fedha kutoka
kwa Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor)… kuna baadhi ya watendaji
wanadai kuwa hizi taarifa ni siri wakati siyo siri,” alisema.
Aliwaeleza
washiriki wa kikao hicho kwamba taarifa hizo ni muhimu kwao kuzipata na
zitawasaidia kuonyesha mapungufu yoyote kama yapo.
Aliwataka kila mmoja wao kwa nafasi zao za Meya na Mwenyekiti wahakikishe wanalenga kupandisha pato la wananchi wanaowaongoza.(A.I)
Post a Comment