Kwa
mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za
Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow
Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo
ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited
(IPTL).
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha
pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo
uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia
nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona wapinzani
wakimwachia suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya
wapinzani. Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke
yake bila kupata kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka
kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.
Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi
maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma. PAC
haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009
iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo
kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na
sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti
ya ‘Tegeta escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana
kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na
kuuzwa kwa TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika
uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco
walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa
uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye
akaunti hiyo maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco
baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu
za mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi
kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na
serikali kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria
kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa
maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha
hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi
zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali
kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada
ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo
kwa kushirikiana na ‘mwekezaji’ aliyechafuka kwa ufisadi duniani?
Serikali
inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma. Umma una
haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata
la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa sasa wa
‘Tegeta Escrow’.
Hoja
nyingine ni kwamba, Mbunge Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa
Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka
akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Nimepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa
na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya ‘Escrow’. Hata
hivyo, nilipopitia muhstasari wa kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara
ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza nikakuta wametafsiri
uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe
kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na
Simba Trust iliyosajiliwa Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya
maamuzi ya kuiba na kugawana wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa
na muhstasari wa kikao vinaambatanishwa).
Wote
waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu ya
Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu
wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na
kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao hicho ndio uliowasilishwa Benki
Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba fedha hizo lazima zitolewa kutoka
akaunti ya Escrow.
Fedha
zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni 250,
katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi
kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha
zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa ni zile
ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio
walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha
zilizotoka kwa walipa kodi.
Ikumbukwe
kwamba uhamishaji wa asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP umeambatana
na nyaraka za kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa uthibitisho wa
cheti halisi cha hisa (share certificate) kutoka kampuni ya Mechmar
kwenda kampuni ya Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha kwamba hisa hizo
(70%) ziliuzwa kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita (6) tu. Na bado
hakuna ushahidi kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa ulipata baraka
za mamlaka husika kama inavyotakiwa na sheria za nchi.
Wakati
huyo anayejiita mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa kuchukua
fedha kutoka akaunti ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki halali
kisheria kwani kodi ililipwa siku moja baada ya wao kupokea fedha kutoka
BoT. Sheria inataka kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA kama
uthibitisho kwamba kodi yote imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya 2012
kifungu cha 29).
Ni
nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu ukawalenga
vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa Wizara ya
Nishati na Madini.
Inapaswa
tutafakari kuona kwamba Harbinder Singh aliyechukua fedha za Escrow,
anamiliki vitalu vya mafuta na gesi kupitia kampuni iitwayo HydroTanz
ambayo nayo imesajiliwa nchini Australia, ikiwa na anwani sawa na ya
kampuni ya Simba Trust. Kitalu hicho cha mafuta kinaitwa ‘Mnazi Bay
North’, jirani kabisa na ugunduzi mkubwa wa hivi karibuni mkoani Mtwara.
Tunatarajia
kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua ukweli wa
sakata hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila kujali
nyadhifa zao serikalini.
Kauli
ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kwamba
kuna watu waliokula rushwa na kwamba nyaraka zinazotajwa ni karatasi za
kuuzia vitumbua, ni kauli zenye kuonyesha kutapatapa kwa watendaji
serikalini. Hakuna hata mahali pamoja ambapo nimemtaja mtu kuwa ni mwizi
zaidi ya kuwasilisha hoja zinazohitaji majibu mwafaka na si matusi,
vitisho na tuhuma za kuzusha. Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za kufungua
maandazi kama ambavyo hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi kuwa
karatasi za kufungia maandazi na badala yake ni nyaraka halali
zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali badala
ya kuropoka na kuporomosha matusi.
Hali
kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji kama Maswi
ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni chombo cha
watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya Bunge. Maswi
na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama yeyote
hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana na
vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua hatua
kama ambavyo vinawachunguza wao.
Kauli
ya Maswi kwamba “wanaume” hawazungumzi ndani ya Bunge si tu
udhalilishaji wa chombo hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume
uliotawala miongoni mwa viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio
wenye hadhi, uwezo na heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili
heshima. Tufumbue macho tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na
itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazalendo ili tuweze
kusimamia utaifa.
1 comments:
When the match will play MICROMAX INDIAN ACES against DBS SINGAPORE SLAMMERS!!
Replyplease tell me..
http://qnique.in/2014/12/08/live-iptl-2014-watch-online-at-starsports-com/
Post a Comment