**********
Dar es Salaam. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko
zito ikieleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kupinga
mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya
Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi Tume ya Mabadiliko
ya Katiba aliyoiteua.
Tamko hilo la CCT ni mwendelezo wa lawama ambazo
Rais Kikwete amekuwa akitupiwa na taasisi na watu mbalimbali kutokana na
mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwenda mrama baada ya mkuu huyo wa
nchi kueleza maoni yake dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Serikali ya
Muungano wakati akilihutubia Bunge la Katiba.
Miongoni mwa watu waliojitokeza kuzungumzia kauli
hiyo katika siku za karibuni ni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa,
John Tendwa, maaskofu wa Kanisa Katoliki, katibu mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif
Hamad.
Jana, CCT iligongomea msumari juu ya lawama hizo
ikifananisha kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa Machi 21, mwaka huu wakati
akifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma na mama anayeamua kubeba
mimba na kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza mtoto, badala ya
kumfurahia.
Pia katika tamko lake (limechapishwa kwa ukamilifu
Uk. 36 wa gazeti hili), jumuiya hiyo imewataka wajumbe wa Bunge hilo
kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuacha
kujadili maoni ya vyama vyao vya siasa.
“Inashangaza jinsi chama kimoja cha siasa
kinavyolazimisha wabunge na wanachama wake kukubaliana na mapendekezo
yake ambayo yanapingana wazi na yaliyomo katika rasimu ya Katiba,”
linaeleza tamko hilo lililotolewa baada ya Mkutano wa 48 wa Halmashauri
Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika Julai 2 na 3 mjini Dodoma.
Tamko hilo pia limetaja mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.
Kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa
ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutoa rasimu ya pili ya Katiba Desemba
30, CCM ilisambaza waraka kuwaarifu wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka
CCM kuwa msimamo wa chama hicho tawala ni Muungano wa serikali mbili,
tofauti na mapendekezo ya wananchi yaliyo kwenye rasimu hiyo ambayo
yanataka serikali tatu.
Licha ya mara kadhaa Jaji Warioba kutetea kile
kilichopendekezwa na Tume yake, wajumbe hao kutoka CCM wameyapinga maoni
hayo na kusisitiza kuwa yanaweza kubadilishwa kadri Bunge la Katiba
litakavyoona inafaa.
Kitendo hicho kilisababisha wajumbe kutoka vyama
vingine kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao Aprili 16
uliamua kususia vikao vya Bunge hilo ukitoa masharti kuwa utarejea
bungeni kama chombo hicho cha kuandika Katiba kitajikita kujadili
mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Bunge hilo litaendelea na vikao vyake Agosti 5 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta anahaha kushawishi Ukawa walegeze msimamo wao.
Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la Katiba,
Rais Kikwete aligusia mambo kadhaa yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na
kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani
kutekelezeka, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali tatu kwa maelezo
kuwa idadi ya watu waliotaka muundo huo ni ndogo.
chanzo na endelea kusoma zaidi : http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/2384004/-/tolp0nz/-/index.html
Post a Comment