Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na ujumbe kutoka Chuo cha
St. Thomas cha Marekani uliomtembelea Ikulu jijini Dar es salaam leo
Julai 16, 2014
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 16 Julai, 2014
amekutana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Thomas cha Minnesota,
Marekani wanaotembelea Tanzania kujifunza uzoefu wa Tanzania katika
masuala ya kiuongozi na anuwai ya tamaduni. Wanafunzi hao ambao kwa
idadi yao ni wanafunzi 14 wanaochukua Shahada za Uzamivu na Uzamivu
katika masuala ya Uongozi wa Kimataifa pamoja na Wakufunzi wao wawili,
Dkt. Jean Pierre Bongila na Dkt. Artika Tyner.
Mkutano huu ni mwendelezo wa mkutano kama huu ambao Katibu
Mkuu Kiongozi aliufanya mwaka jana na kundi jingine la wanafunzi kutoka
Chuo hicho ambapo aliwapa uzoefu wa uongozi na anuwai ya tamaduni katika
Tanzania, Afrika na katika medani za kimataifa.
Kwa
kutambua umuhimu wa nasaha walizozipata wanafunzi wa mwaka jana, Chuo
hicho kiliomba na kukubaliwa fursa nyingine ya kuonana na Katibu Mkuu
Kiongozi. Ziara ya wanafunzi hao ilianzia Arusha tangu tarehe 12 Julai,
2014 na itamalizika tarehe 17 Julai, 2014.
Pamoja
na kupata fursa ya kuonana na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa
wa Arusha, wanafunzi hao walipata pia muda wa kutembelea vivutio
mbalimbali vya utalii vilivyopo Arusha na baadaye Zanzibar. Na matarajio
ni kuwa wanafunzi hao watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania
sehemu mbalimbali za dunia watakakokwenda kufanya kazi.
Kwa
ujumla, wanafunzi wamepata fursa nzuri ya kuuliza maswali yaliyogusa
maeneo yote yanayohusu uongozi, siasa, uchumi, elimu, afya na utamaduni
ambayo yalipata ufafanuzi wa kutosha kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Post a Comment