Hai. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (pichani) ameingia matatani
baada ya Mahakama ya Wilaya ya Hai kuona ana kesi ya kujibu katika
mashtaka ya kumshambulia mwangalizi wa ndani katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010.
Uamuzi huo ulitolewa jana na hakimu mfawidhi wa
wilaya hiyo, Denis Mpelembwa mbele ya Mbowe, wakili wake, Issa Rajabu na
mwendesha mashtaka, Inspekta Marwa Mwita.
Mpelembwa alisema mashahidi saba wa upande wa
mashtaka wameishawishi mahakama kuwa siku hiyo kuna tafrani ambayo
ilitokea na ambayo Mbowe
Alisema ingawa upande wa utetezi ukiongozwa na
wakili Albert Msando na baadaye Rajabu, ulitoa hoja kuwa ushahidi wa
Jamhuri uliacha mashimo mengi, yeye anaona Mbowe ana kesi ya kujibu.
“Katika hoja zao (utetezi) wanaona ukiacha
ushahidi wa Nassir Yamin, hakuna shahidi mwingine aliyethibitisha
kushuhudia Nassir akipigwa,” alisema akinukuu hoja za mawakili wa
utetezi.
Hakimu aliongeza kusema: “Utetezi pia walitoa hoja
kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwaita akina mama ambao wanaodaiwa
kushuhudia, hivyo kuacha mashimo mengi katika ushahidi wao.”
Hata hivyo, hakimu alisema katika hoja zao ambazo
ziliishawishi mahakama, upande wa mashitaka ulijibu kuwa sheria
haiwabani kuleta kila shahidi kujenga msingi wa kesi yao.
“Ni rai yao (mashtaka) kuwa mashahidi wao saba
wameweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha mashaka
ama mianya kama utetezi walivyodai,” alisema Mpelembwa.
Hakimu Mpelembwa alisema baada ya kupitia hoja za
mawakili wa pande zote mbili, anaona upande wa Jamhuri umeweza
kuishawishi mahakama kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
Kutokana na uamuzi huo, Hakimu alisema mahakama
inampa nafasi Mbowe kujitetea na kesi hiyo imepangwa kutajwa Julai 17,
siku upande wa utetezi utakapotoa orodha ya mashahidi wao.
Katika uchaguzi huo mkuu wa 2010, Mbowe aliibuka
mshindi kwa kupata kura 28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM), kura
23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment