
Ndugu zangu,
Nimeandika
juzi, kuwa nchi yetu haina uhaba wa wagombea urais, na kwenye moja ya
magazeti ya leo, wametajwa wanaoweza kugombea kuwa ni kumi na mmoja,
kama kikosi cha kucheza mechi kwenye Kombe la Dunia!
Si
kugombea tu, kwamba kimsingi yeyote anaweza kugombea Urais. Kwenye siku
ya Saba Saba mwaka huu nilikuwa kijijini Idodi, Pawaga. Pale niliwaona
watoto hao pichani wakisubiri kwa hamu kuongalia kitakachoonyeshwa
kwenye KwanzaJamii Cinema. Ilikuwa ni marudio tu ya mechi za Kombe la
Dunia, lakini, wengi walikusanyika, kuangalia.
Kwa
kuangalia watoto hao nilitafakari sana kuhusu nchi yetu, kwamba pamoja
na hali duni za watu wetu wengi, yumkini tuna Watanzania miongoni mwetu
wenye ndoto za kuwa marais kwa kudhani ni kazi rahisi sana, na kwa nchi
yetu, hakuna pia uhaba wa ndoto za urais. Tatizo letu kama Taifa ni
ukweli kuwa hatuna NDOTO ya TAIFA. Kwamba tunataka nini kama taifa.(P.T)
Na kama
tungelikuwa na ndoto ya taifa, basi, na wenye ndoto za urais nao
wangepungua, maana, mwenye kuota ndoto ya urais angelazimika pia
kujiuliza swali muhimu; " Je, mimi natosha kwenye kuyatimiza yale
yaliyomo kwenye ndoto ya taifa?"
Na kwa
vile hatuna ndoto ya taifa, tusije tukashangaa siku moja, kuwa idadi ya
watakaochukua fomu kugombea urais kufikia hata idadi ya kikosi
kinachoruhusiwa na FIFA kwenda kushiriki kwenye fainali za Kombe la
Dunia; wachezaji 23, hivyo basi, wagombea urais 23!
Ni Neno Fupi La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Iringa.
Post a Comment