Nyumba-kigoma
Pichani ni sehemu ya nyumba iliyoteketezwa na moto na wananchi wenye hasira kali wa kijiji cha Lugongoni “A” Kata na Tarafa ya Nguruka wilayani Uvinza mkoani Kigoma kwa kile kinachodaiwa ni imani za kishirikina.

Na Mwandishi wetu, Kigoma

Familia nne za wakazi wa Kijiji cha Lugongoni “A” Kata na Tarafa ya Nguruka Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma, hazina makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto na nyingine kubomolewa na kundi la wananchi wa kijiji hicho kutokana na imani za kishirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Frasser Kashai, alisema kuwa tukio la nyumba za wakazi hao kuchomwa na kubomolewa limetokea Julai 13 mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi kijijini hapo ambapo nyumba mbili zilichomwa moto na nyingine mbili kubomolewa.

Alitaja familia za watu walioathirika kuwa ni familia ya Siwajui Ahamad, Ahamad Ramadhani, Abdalah Ahamad na Mayila Ahamad ambao nyumba zao zote zimeteketea kwa moto na hakuna kilichookolewa.

Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni imani potofu za kishirikina ambapo mtu mmoja aitwaye Masoud Vyombo alifariki Julai 10 na kuzikwa Julai 11, lakini mnamo Julai 12 mwanamke aitwaye Siwajui Ahamad alifika msibani na wananchi kumtuhumu kuhusika na kifo hicho na hivyo kumshambulia kwa lengo la kumuua.

“Mwenyekiti wa Kitongoji aitwaye Matei Joseph alijitahidi kumwokoa mwanamke huyo na baada ya kumwokoa wananchi hao walijichukulia sheria mkononi na kwenda kuchoma moto nyumba yake moja na nyingine moja pia ikachomwa moto na mbili kubomolewa,”alisema Kashai.

“Nyumba zote zilizochomwa moto na zilizobomolewa ni za watu wa familia moja na thamani ya mali zilizoharibiwa bado haijafahamika.”

Aidha Kamanda Kashai alisema kuwa watu 15 tayari wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo kwa mahojiano na upelelezi na itakapothibitika kuhusika katika tukio hilo kutokana na ushahidi watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kuhusu usalama wa watu waliochomewa na kubomolewa nyumba zao, kamanda Kashai alisema kuwa baadhi wamehifadhiwa katika kituo cha Polisi Uvinza na wengine wako kwa ndugu zao wakati taratibu nyingine zikiendelea.