NA MWANDISHI WETU, DODOMA
KAMATI
Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya
Mwenyekiti wake Philip Mangula, imeanza vikao vyake mjini Dodoma kupitia
taarifa za utekelezaji wa adhabu kwa makada sita wa chama hicho
wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais mwaka 2015 kabla ya wakati.
Chanzo
cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kiliiambia MTANZANIA kuwa kikao hicho
kilianza jana saa 6 mchana, kuanza kupata taarifa za kamati za maadili
za mikoa.(I.N)
Hatua
hiyo inatokana na agizo la Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa
CCM, alilolitoa Februari 8, mwaka huu kwa kuzitaka ofisi zote za ngazi
ya mikoa na wilaya kufungua mafaili hayo ili kupitia mienendo ya
wagombea walioanza kampeni za uchaguzi wa kuteuliwa kugombea urais kabla
ya wakati.
Makada
hao waliozuiwa kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku mienendo yao ya
kisiasa ikifuatiliwa ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine
ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja.
"Leo
(jana) tangu saa 6 mchana Kamati Ndogo ya Maadili ilikuwa na vikao
mfululizo, na kazi kubwa walikuwa wanapitia mafaili ya wagombea
waliotangaza nia ya kuwania urais mwaka 2015.
"Walichokuwa
wanakifanya ni taarifa ya utekelezaji wa adhabu hiyo kwa kila mgombea
pamoja na kufuatilia mienendo yao... ila kinachoonekana kuna baadhi ya
makada huenda adhabu zao zikaongezwa na hata kupoteza sifa za kuwania
nafasi hiyo.
"Unajua
tangu walipopewa adhabu, baadhi yao wamekuwa wakikiuka na hata kuendelea
na mikakati ya kampeni kwa kukusanya watu wao kupanga nini cha kufanya
kuelekea mwaka 2015, pia wengine walitumia Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani
kuandaa futari ambazo zilikuwa na harufu ya kampeni," kilisema chanzo
hicho kilichopo Makao Makuu ya CCM Dodoma.
Taarifa
kutoka ndani ya kikao hicho cha Kamati Ndogo ya Maadili na Nidhamu,
zinaeleza kuwa katika kipindi cha miezi kadhaa, timu za maofisa usalama
wa chama zilisambazwa mikoa yote na kukusanya taarifa za makada hao.
Kikao
hicho kimefanyika kabla ya kuanza kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC),
kilichoitishwa kwa dharura mjini hapa leo chini ya Mwenyekiti wake Rais
Jakaya Kikwete.
Hatua
hiyo ya kuitishwa kikao hicho imekuja baada ya kuwapo kile kinachodaiwa
ni shinikizo kutoka kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kumtaka
Rais Kikwete aliahirishe Bunge la Katiba linaloendelea na vikao vyake
mjini hapa.
Hatua ya
Rais Kikwete kuitisha CC inatokana na uamuzi wa kamati hiyo, iliyoketi
Julai 16, mwaka huu ambapo ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya
wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea
urais.
Kutokana
na hali hiyo, CC iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia
utekelezaji wa adhabu kwa makada hao sita kama wanatekeleza ama la.
Hatua
hiyo ya CCM kupitia mienendo ya makada hao waliopewa onyo Februari mwaka
huu inawafanya kukalia kuti kavu, kwani ikiwa watabainika kuvunja
utaratibu wa chama wanaweza kupoteza sifa za kuwania urais mwakani.
Julai 17,
mwaka huu Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema
endapo Kamati ya Usalama na Maadili itabaini kama makada hao walikiuka
mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa, watapoteza sifa.
Kabla ya
adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili
ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na
Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara ya 6 (7)(i).
Nape
alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama
wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais.
"Baada ya
kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili
wasipoteze nia ya kugombea, ni muhimu wakazingatia Katiba, kanuni na
taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo," alisema Nape.
Alisema
kama itabainika makada hao hawakutekeleza masharti ya adhabu zao kama
zilivyotolewa na CC, kuna hatari ya kuongezewa adhabu kulingana na
ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
"Kila
mmoja anafuatiliwa mwenendo wake, kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati
Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za chama kwa suala hili,
Kamati ya Usalama na Maadili ya chama itafanya mapitio ya mwenendo wao
wa utekelezaji wa adhabu hiyo.
"Kama
watakuwa hawajatekeleza adhabu zao, kamati itapeleka mapendekezo CC ili
waweze kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa makosa yao na taratibu
za chama," alisema Nape.
Alisema
ni muhimu kwa wanachama wote kukumbuka chama ni pamoja na Katiba, kanuni
na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga jambo
ambalo halivumiliki.
Kwamba
nia ya CCM ni kusimamia na kuhakikisha chama kinakuwa na umoja na
mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa katika kuelekea kukamilisha kazi
ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu
mwaka 2015.
Habari
ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Kamati Kuu, zinasema
aliyetoa hoja kuendelea kufuatiliwa kwa makada hao ni Makamu Mwenyekiti
wa CCM-Bara, Mangula aliyesema amefungua faili kwa ajili ya makada hao.
Alisema suala jingine alilowasilisha Mangula ni ripoti ya ziara yake aliyoifanya katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Tanga.
Februari
18, mwaka huu CCM kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika
kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makada wake
ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
Uamuzi huo ulibarikiwa na Kamati Kuu iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete
CHANZO:MTANZANIA
Post a Comment