Vilio na simanzi jana vilitawala kwa wakazi wa maeneo ya Sinai-Mabatini, baada ya vifo vya watu wanne wa familia mbili tofauti, vilivyotokana na mvua iliyosababisha miamba mikubwa ya mawe kuporomoka na kuponda nyumba zao usiku wa manane.
Tukio
hilo la kusikitisha limeripotiwa kutokea saa nane usiku kuamkia jana,
wakati mvua iliyoambatana na upepo wa wastani ilipokuwa ikiendelea
kunyesha, na
kusababisha miamba hiyo mikubwa inayokadiriwa kufikia tani mbili
kuporomoka na kuziponda nyumba hizo na kusababisha vifo hivyo na
majeruhi wanne.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa
mvua.
Mpekuzi ilifanikiwa kufika eneo la tukio na kushuhudia
miamba hiyo ikiwa imeharibu nyumba, huku nyumba moja iliyojengwa kwa
matofali ya tope ikiwa imeanguka na kubaki kifusi.
Nyumba zilizokumbwa na maafa hayo zinamilikiwa na watu waliotajwa kwa
majina ya Joseph William na Lameck Ajiji, na kila moja watu wawili
wamefariki kwa kukandamizwa na miamba hiyo.
Katika nyumba ya William iliyokuwa na watu watano, waliofariki
wametajwa kuwa ni Kefa Joseph (15) na Emmanuel Joseph (12), wote wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani na majeruhi mmoja ambaye
hakufahamika jina lake ambaye alikimbizwa hospitali.
Nyumba inayomilikiwa na Ajiji yenye watu watatu, waliofariki
wametambuliwa kuwa ni mama wa nyumba hiyo, Kwinta Geko (24) na mumewe
Samson Odinya.
Waliojeruhiwa ni mtoto Bety Samson (4) na Godfrey Joseph (14) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani.
Tukio hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo la Sinai. Mara ya
kwanza ilikuwa ni mwaka 2009 baada ya miamba kuporomoka na kusababisha
vifo vya watu wawili wa familia moja.
Mamia ya wananchi waliofika eneo hilo, walijitolea kwa kumpa fedha mtoto Bety aliyenusurika kufa kutokana na tukio hilo.
Mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (Chadema), alifika
eneo la tukio na kutoa pole kwa wananchi, ndugu jamaa na marafiki wa
familia zilizoathirika na janga hilo, ambapo alionyesha kushtuka baada
ya kuelezwa na wananchi kwamba hakuna kiongozi yeyote wa Serikali
aliyefika eneo hilo.
Akizungumza kwa kutumia kipaza sauti mbele ya umati wa watu waliokuwa
wamefurika katika eneo hilo la tukio, alisema: “Inashangaza sana kuona
hata mkuu wa wilaya hajafika hapa. Nitawasiliana na viongozi wa Serikali
na mchana nitarudi hapa tena.”
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwandishi katika eneo la
tukio, waliiomba Serikali kuzuia wananchi kujenga karibu na miamba
mikubwa, kwani kufanya hivyo itasaidia sana kuepusha maafa kama hayo.
“Kwa kweli tukio hili linasikitisha sana, na tunaomba viongozi wa
serikali wasaidie wananchi kuwaondosha kwenye maeneo ya kwenye miamba,”
alisema mmoja wa wananchi hao ambaye pia ni balozi wa Shina Namba Tano,
Mtaa wa Nyerere A, Jackson Kitundu.
Post a Comment